Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wakazi wa kijiji cha Usinge Wilayani Kaliua wakati wa ziara yake ya siku mbili kufuatilia utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Tabora mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Mbunge wa Kaliua Dkt Aloyce Kwezi
Sehemu ya wakazi wa kijiji cha Usinge wilaya ya Kaliua mkoa wa Tabora wakimskiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
Mbunge wa Jimbo la Kaliua Dkt Aloyce Kwezi akizungumza katika mkutano wa wakazi wa kijiji cha Usinge wilayani Kaliua mkoa wa Tabora na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula mwishoni mwa wiki.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsikiliza Mpima wa mkoa wa Tabora Bakari Zema wakati akikagua maeneo yatakayoendeshwa mradi wa upimaji katika halmashauri ya wilaya ya Kaliua mkoa wa Tabora mwishoni mwa wiki.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi hati za umiliki ardhi Mkuu wa wilaya ya Urambo Louis Bura wakati wa ziara yake ya siku mbili kufuatilia utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Tabora mwishoni mwa wiki.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua mkoani Tabora aliowakabidhi hatimiliki za ardhi wakati wa ziara yake ya siku mbili kufuatilia utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani humo mwishoni mwa wiki. (PICHA NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)
******************************
Na Munir Shemweta, WANMM KALIUA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka wamiliki wapya wa ardhi nchini kuzingatia masharti ya umiliki ikiwemo kuendeleza maeneo wanayomilikishwa katika kipindi cha miezi 36.
Aidha, amewataka wamiliki hao kuhakikisha wanalipa kodi ya pango la ardhi kila mwaka ili kuepuka kutozwa riba sambamba na kuwa wadaiwa sugu wa kodi hiyo.
Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Usinge wilayani Kaliua mkoa wa Tabora mwishoni mwa wiki Dkt Mabula alisema, ni vizuri wamiliki wapya wa ardhi mara tu wanakabidhiwa hati za umiliki ardhi wakasoma masharti ya umiliki ili kuelewa na kuepuka kuingia kwenye matatizo yanayoweza kusababisha kunyang’anywa ardhi.
‘’Wamiliki wapya wa ardhi ni vizuri mnapokabidhiwa hati mkasoma masharti ya uimiliki ardhi na moja ya masharti ni kuendeleza kiwanja chako katika kipindi cha miezi 36 na msipozingatia masharti mtaingia kwenye matatizo na watu wa ardhi’’ alisema Naibu Waziri Mabula.
Dkt Mabula aliwataka wakazi wa kijiji cha Usinge wilayani Kaliua kuchangamkia zoezi la urasimishaji makazi holela kwenye maeneo yao ili waweze kumilikishwa na kuzitumia hati katika shughuli za maendeleo.
‘’Ndungu zangu wa Usinge Serikali inakuja kupima maeneo yenu na hii ni fursa kwenu hivyo nawaomba mchangamkie zoezi hili maana hapa gharama ni shilingi 50,000 kiasi ambacho ni kidogo sana ukilinganisha na maeneo mengine, Tabora manispaa wanalipa 130,000 katika zoezi la urasimishaji‘’ alisema Dkt Mabula.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Tabora Jabir Singano, katika mkoa mzima wa Tabora halmashauri za Uyui na Kaliua ndiyo halmashauri pekee ambazo kwa muda mrefu hazikuwa na mradi wa upimaji na ofisi yake imependekeza kupatiwa fedha kwa ajili ya mradi wa kupanga na kupima kwenye halmashauri hizo.
‘’Tayari kazi ya kupima viwanja 1000 hapa katika kijiji cha Usinge, Kaliua imeshaanza na tunasubiri hela iingie kwenye akaunti ili kazi ya kupima kule Uyui na Manispaa ianze’’ alisema Singano.
Halmashauri ya wilaya ya Kaliua mkoani Tabora imepanga kupima jumla ya viwanja 1000 eneo la Usinge ikiwa ni sehemu ya mkopo wa shilingi bilioni 50 zilizotolewa na serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuzikopesha halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya miradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi (KKK) kwenye maeneo yake.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula alizionya halmashauri kutozitumia fedha hizo nje ya shughuli iliyokusudiwa na kufafanua kuwa matumizi yoyote kinyume na malengo yake kutazifanya halmashauri hizo kushindwa kufikia malengo yake.
‘’Isitoke hata senti moja ikaenda katika malipo ya mahitaji mengine na mkifanya hivyo mtashindwa kufikia lengo kwa hiyo muandae mpango wa utekelezaji mradi huo wa upangaji na upimaji na kupitia taratibu zote’’ alisema Dkt Mabula.
Mbunge wa jimbo la Kaliua ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Dkt Aloyce Kwezi aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Ardhi kwa kuikopesha halmashauri ya Kaliua fedha za mradi wa upimaji ardhi na kuongeza kuwa maendeleo kwenye jimbo lake sasa yanaenda kwa kasi.
‘’Maendeleo katika wilaya ya Kaliua yanaenda kwa kasi na niishukuru serikali kwa kutupatia fedha za miradi mbalimbali ukiwemo huu wa upimaji na nichukue fursa hii pia kulishukuru Shirika la Nyumba la Taifa kwa kutupatia milioni 10 kwa ajili ya shule zetu mbili za Kasunga na ile ya Dkt John Pombe Magufuli’’ alisema Dkt Kwezi.
Katika ziara yake mkoani Tabora, Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula alitembelea pia halmashauri za Manispaa ya Tabora na Urambo na kuzungumza na watumishi wa sekta ya ardhi ambapo aliwataka kuongeza kasi ya utoaji hati na kuingiza viwanja kwenye mfumo wa utunzaji kumbukumbu za ardhi ili kuweza kuwafuatilia wamiliki na kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi.
0 Comments