Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano la Uwekezaji lililofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar leo tarehe 7 Desemba, 2021.
Waziri wa Uwekezaji, Mhe. Geoffrey Mwambe akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano la Uwekezaji lililofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar leo tarehe 7 Desemba, 2021.
Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Amani Abeid Karume akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano la Uwekezaji lililofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar leo tarehe 7 Desemba, 2021.
*****************************
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefungua Kongamano la Uwekezaji lililofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar leo tarehe 7 Desemba, 2021.
Akihutubia viongozi, wageni na wananchi waliohudhuria kongamano hilo, Mhe. Mwinyi amesema kwamba Kongamano la Maonesho ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania yatakayoendelea hadi tarehe 9 Desemba, 2021 ni maalum katika kutathmini mafanikio na changamoto za maendeleo za shughuli za uwekezaji wakati huu Tanzania ina adhimisha Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Mhe. Rais amezungumzia kongamano hilo kuwa kama njia moja wapo ya kujadili fursa zilizopo katika kilimo, madini, ujenzi wa miundombinu, usafirishaji, afya, elimu pamoja na maeneo maalum yaliyopewa kipaumbele na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikiwemo Uchumi wa Bahari.
"Katika kufanikisha utekelezaji wa Uchumi wa Bluu ambao ni ajenda yetu maalum, Serikali inawakaribisha wawekezaji katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayohusiana na uchumi huo wa bahari ikiwemo ujenzi wa bandari kubwa ya kisasa ya Mangapwani ambayo itajumuisha bandari ya mafuta na gesi, bandari ya nafaka na chelezo kwa ajili ya matengenezo ya meli." amesema Rais Mwinyi
Aidha Mheshimiwa Rais amasema kuwa kutokana na mafanikio yaliyopatikana kujenga uchumi, Serikali zote mbili zina wajibu wa kuendeleza mipango ya waasisi na viongozi wote wa awamu zilizotangulia kwa kuweka misingi ambayo uongozi wa Serikali zilizopo zinaiendeleza na kuimarisha zaidi.
"Miongoni mwa mafanikio yetu ni kuwepo kwa sera na mipango endelevu ya uwekezaji ili kujenga mazingira bora yanayowavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi." ameongezea Rais
Nae Waziri wa Uwekezaji, Mhe. Geoffrey Mwambe amesema kuwa Serikali imejidhatiti katika kuangalia maeneo ya uwekezaji ili kuweza kujenga msingi mkuu wa uchumi wa nchi yetu.
"Kupitia uwekezaji, ndio tunajenga uwezo mkubwa, uwezo mpana wa kuzalisha ili pato la taifa liongezeke." amasema Mhe. Mwambe.
0 Comments