Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Jokate Mwegelo akijaza mafuta katika daladala inayofanya Safari zake kati ya Temeke na Stesheni, akiashiria kuzindua rasmi Wiki ya Huduma kwa Wateja wa Puma Energy Tanzania.Wengine wanaoshuhudia ni maofisa kutoka Puma wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Lameck Hiliyayi.Uzinduzi huo umefanyika leo katika cha mafuta cha Puma kilichopo Sokota.
* Yazindua wiki ya wateja na kituo kipya cha mafuta Sokota, Temeke
KAMPUNI ya Mafuta ya Puma Energy Tanzania imepongezwa kwa ushirikiano mkubwa unaotoa kwa serikali kupitia ajira wanazotoa kwa vijana kupitia vituo vyao vya mafuta vinavyopatikana kote nchini.
Hayo yameelezwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo wakati akizindua wiki ya huduma kwa wateja kwa mwaka 2021 pamoja na kuzindua kituo kipya cha mafuta kilichopo Sokota, Temeke jijini Dar es Salaam.
''Puma wanaongoza kwa huduma nzuri na bidhaa bora za mafuta na vilainishi ambavyo vina viwango vya kimataifa vyenye kukidhi mazingira na watumiaji wake, na katika kukabiliana na soko la ajira Puma Energy wamekuwa wakishirikiana na Serikali kwa ukaribu zaidi kwa kutoa ajira kwa kundi kubwa la vijana na ajira hizo zina miiko na maslahi kwa wafanyakazi wake......Huu ni mfano wa kuigwa, Ofisi yangu licha ya kupokea malalamiko mengi ya wafanyakazi hatujawahi kupokea malalamiko yoyote kutoka wafanyakazi wa kampuni ya Puma Energy tunawapongeza kwa hili.'' Amesema Jokate.
Amesema, Puma Energy Tanzania pia imekuwa ikishiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi jambo linaloungwa mkono na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mamlaka za TARURA, na TANROAD kwa kuwaelimisha wanafunzi na jamii kwa ujumla kupitia kampeni mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zinapunguza ajali za barabarani zinazosababisha vifo na ulemavu.
Jokate ameeleza ongezeko la vituo vya Puma hasa katika maeneo ambayo hayakufikiwa na huduma hiyo kunakwenda sambamba na azma ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan yenye mlengo katika uwekezaji na kuzalisha ajira kwa watanzania.
Kuhusiana na wiki ya huduma ya wateja, Jokate amesema kampuni hiyo imekuwa ikijali watanzania kupitia bidhaa zao za mafuta, vilainishi na maduka yanayopatikana katika vituo vyao na kupitia wiki hiyo ya wateja watapata matokeo chanya ya kuboresha huduma zao baada ya kusikiliza maoni na mapendekezo kutoka kwa wateja wao.
Vilevile DC Jokate ametumia wasaa huo kuwakaribisha wakazi wa Temeke na wana Dar es Salaam kuhudhuria maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru na kumshuhudia Rais wa kwanza Mwanamke Rais Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride katika siku hiyo adhimu kwa watanzania.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Kaimu Mkurugenzi wa Puma Energy Tanzania Lameck Hiliyayi amesema, kampuni hiyo ina ubia na Serikali kwa asilimia 50 kwa 50 na kipaumbele chao ni kutoa huduma bora kwa wateja kupitia bidhaa za mafuta, vilainishi na maduka yanayopatikana katika vituo vyao vya mafuta.
Amesema, katika maadhimisho hayo yaliyobebwa na kauli mbiu ya 'Huduma Nzuri kwa Wateja' wateja watapata fursa ya kutoa maoni yao, mapendekezo, ushauri pamoja na kujishindia zawadi mbalimbali na kueleza kuwa tangu kuanzishwa kwa wiki hiyo ya wateja 2019 wamekuwa wakipata manufaa mengi kupitia wateja wao.
Vilevile amesema, wamekuwa wakishirikiana na Serikali kwa ukaribu katika kutatua changamoto ya ajira.
''Tumekuwa tukishirikiana na Serikali kwa ukaribu zaidi katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana, tumeajiri vijana wengi katika vituo vyetu vya mafuta, walinzi na wafanyakazi katika maduka yote ya Puma Energy na hii ni kwa vituo vyote nchini.'' Amesema.
Awali Meneja wa Mauzo ya rejareja wa Puma Energy Tanzania Bi. Venessy Chilambo amesema, wiki ya huduma kwa wateja ni fursa kwao kwa kuchukua mrejesho kutoka kwa wateja na kuifanyia kazi ili kuboresha huduma na maadhimisho hayo yanaadhimishwa katika vituo vyao vyote.
Venessy amewashauri wateja na watanzania kwa ujuma kutumia bidhaa na kufurahia huduma zinazotolewa na kampuni hiyo kwa usalama wao binafsi na vyombo vya moto
Matukio Mbalimbali katika hafla ya uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja ya Kampuni ya mafuta ya Puma Energy Tanzania.
0 Comments