Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) (kulia) akitunuku vyeti katika Mahafali ya 47 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Kampasi ya Dodoma, yaliyofanyika jijini Dodoma, katikati ni Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Imanueli Mnzava.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) (kulia) akiwataka wahitimu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Kampasi ya Dodoma kujiepusha na vishawishi vya rushwa, wakati wa Mahafali ya 47 ya Chuo hicho, yaliyofanyika jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) (kulia) akiwa katika maandamano wakati wa Mahafali ya 47 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Kampasi ya Dodoma, yaliyofanyika jijini Dodoma, kushoto ni Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Imanueli Mnzava.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu katika Mahafali ya 47 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Kampasi ya Dodoma, yaliyofanyika jijini Dodoma, kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo hicho, Prof. Emmanuel Mjema na kushoto ni Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Imanueli Mnzava.
Wahitimu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Kampasi ya Dodoma wakiwa tayari kutunukiwa Astashahada na Shahada za Uzamili katika fani ya Benki, Fedha na Uwekezaji, jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM)
***************
Na. Peter Haule, WFM, Dodoma
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amekitaka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kuwatumia wataalamu wake katika kufanya tafiti katika nyanja za usimamizi wa fedha, uhasibu na Sheria za mifumo ya Fedha pamoja na teknolojia ili kuimarisha uweledi utakaosaidia wananchi na Serikali kukabiliana na changamoto katika sekta ya fedha.
Amebainisha hayo wakati wa mahafali ya 47 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha Kampasi ya Dodoma yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mhandisi Masauni alisema Chuo hicho kinatakiwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kupeana na kubadilishana maarifa kwa kuwa dunia ya sasa ni ya teknolojia na utandawazi.
“Tunahitaji wataalam wenye weledi, maarifa na umahiri wa kutatua changamoto na si kuongeza changamoto. Zingatieni kwa umakini suala la umahiri katika mitaala yenu ili tuweze kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kuleta mabadiliko kiuchumi”, alieleza Mhandisi Masauni.
Alisema kuwa ni matarajio ya Serikali kukiona Chuo hicho kinaendelea kutoa wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa ili kukabiliana na changamoto ya ajira iliyopo duniani kote na hatimaye waweze kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Alisema ni jukumu la Chuo kuboresha mitaala na kujikita kwenye kuyafahamu mahitaji ya soko kwa kutoa mafunzo yanayowaandaa wahitimu wanaokidhi mahitaji ya soko kwa kuzingatia mapinduzi ya viwanda ili kuhakikisha taaluma na nyenzo wanazozitoa kwa wanafunzi zinaendana na mahitaji ya soko.
Aidha amewaasa vijana wote wa kitanzania waliomaliza elimu zao za juu hivi karibuni kutumia taaluma waliyoipata katika utendaji kwa kuwa walikuwa katika mafunzo kwa nadharia na wanaingia katika ulimwengu wa utekelezaji kwa vitendo, hivyo elimu waliyoipata darasani haitakuwa na maana kama watashindwa kuitafsiri katika uhalisia wa mazingira yanayowazunguka.
Alisisitiza kuwa vijana wanatakiwa kufanya kazi kwa haki, bidii, uadilifu, ubunifu, uaminifu, umakini, weledi na kujiepusha na uzembe na kufuata msingi mkuu wa mafanikio ambao ni kufanya kazi kwa kuzingatia Sera, Sheria, Taratibu na Kanuni zilizowekwa.
Pia amewataka kujiepusha na vishawishi au vitendo vyovyote vya rushwa, ubadhirifu na vingine visivyo halali na kuwa wakumbuke kuwa rushwa ni adui wa haki na maendeleo ya Taifa.
Naibu Waziri Mhandisi Masauni, amekipongeza Chuo cha IFM kwa hatua mbalimbali inazochukua kusogeza huduma zake karibu na wananchi ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kampasi ya Chuo hicho Jijini Dodoma pamoja na mikoa mingine ikiwemo Mwanza na Simiyu.
Wahitimu katika Mahafali ya 47 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha, jijini Dodoma ni pamoja na wale wa astashahada ya uhasibu, Benki na Fedha na Shahada ya Uzamili katika fani ya Fedha na Uwekezaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha IFM, Prof. Emmanuel Mjema, alisema kuwa katika mwaka 2020/2021 Chuo kimeanza kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano ambao umetayarishwa kuendana na Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano wa Taifa.
Alisema kuwa Mpango huo umeainisha malengo makuu ikiwa ni pamoja na kuboresha mafunzo ya kitaaluma na kitaalamu, utafiti na ushauri elekezi, lakini pia kuboresha michakato ya biashara na utawala na kuzingatia sera ya kitaifa juu ya magonjwa ya kuambukiza.
0 Comments