Ticker

6/recent/ticker-posts

BODI YA MAABARA BINAFSI WIZARA YA AFYA YAWAPIGA MSASA WARATIBU WA MAABARA WA HALMASHAURI.


***************************

Na Rayson Mwaisemba WAMJW-DODOMA.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Bodi ya Maabara Binafsi imeendelea kutoa mafunzo kwa Waratibu wa huduma za Maabara ngazi ya Halmashauri ili kuwajengea uwezo juu ya namna bora ya kusimamia na kuboresha huduma zinazotolewa na Maabara Binafsi za Afya nchini.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanayoendelea Jijini Dodoma yamefunguliwa leo na Msajili wa Maabara Binafsi za afya kutoka Wizara ya Afya Bw. Dominic Fwiling’afu aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe.

Katika mafunzo hayo Msajili wa Maabara Binafsi Bw. Dominic Fwiling’afu amesema, katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi, mnamo mwaka 1997 Serikali ilipitisha Sheria Sura 136 ya kusimamia utoaji wa huduma za Maabara Binafsi za Afya Lengo ni kuhakikisha huduma zinatolewa na maabara binafsi za afya zinakidhi vigezo na kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.

“Katika jitihada za kuimarisha upatikanaji na utoaji huduma za afya kwa wananchi, mnamo mwaka 1997 Serikali ilipitisha Sheria Sura 136 ya kusimamia utoaji wa huduma za Maabara Binafsi za Afya ili kuhakikisha huduma zinatolewa na maabara binafsi za afya nchini zinakidhi vigezo na kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.” Amesema.

Amesema, katika mafunzo haya waratibu watapata fursa ya kupitishwa kwenye changamoto mbalimbali zilizobainika kwenye kaguzi zilizofanywa na Bodi kwenye Mikoa mbalimbali na kuweka mikakati ya pamoja ya kuweza kuzitatua changamoto hizo ili kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Bodi.

Aidha, Bw. Fwiling’afu amesema kuwa, mafanikio yatakayopatikana baada ya kikao hiki yatasaidia kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma bora za Afya nchini, kwani huduma hizi zina umuhimu wa pekee katika kutambua vyanzo vya magonjwa na matibabu yake kisayansi.

”Mafanikio yatakayopatikana baada ya kikao hiki ni wazi kuwa yatachangia kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma bora za Afya nchini, ikizingatiwa kuwa, huduma za maabara zina umuhimu wa pekee katika kutambua vyanzo vya magonjwa na matibabu yake.” Amesema.

Mafunzo haya yanayotolewa na Bodi yakawe chachu kwenu kuhakikisha maabara binafsi zote mnazosimamia zinatoa huduma zenye viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa, kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na miongozo yote inayotolewa na wizara ya Afya inayohusu uanzishwaji na usimamiaji wa huduma bora za Maabara Binafsi za Afya ili wagonjwa wapate tiba sahihi na kwa wakati, amesisitizi Bw. Fwiling’afu.

Mbali na hayo, ameweka wazi kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya inatarajia kuona mabadiriko makubwa baada ya mafunzo haya ikiwemo kutumia wataalamu wenye sifa na kuzingazia kanuni na miongozo ya utoaji wa huduma, Maabara Binafsi za Afya zote nchini kusajiliwa na Bodi ya Maabara Binafsi za Afya, kulipa ada za mwaka kwa wakati, Maabara binafsi za afya zote zinaorodheshwa kwenye mfumo wa usajili wa vituo (HFRS) ili Kuimarisha utunzaji na upatikanaji wa taarifa.

Nae, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za dawa OR. TAMISEMI Bw. Mathew Mganga ametoa wito kwa Waratibu wa Maabara wa Halmashauri zote nchini kuwa kichocheo cha kukuza taaluma ya huduma za maabara ili wananchi wapate huduma bora na kwa wakati, hali itayoijengea taswira nzuri Serikali inayosimamia huduma hizo.

Pia, amewataka Wataalamu hao kusimamia utoaji huduma za maabara kwa kufuata kanuni, miongozo, taratibu na Sheria za utoaji huduma za maabara bila kumwonea mtu ili kuondoa kero na malalamiko kuhusu huduma kutoka kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments