Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kiarabu (BADEA) Dkt. Sidi Ould Tah baada ya Benki hiyo kuahidi kuipatia Tanzania mikopo yenye masharti nafuu pamoja na misaada inayokadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni tatu sawa na shilingi trilioni 7 katika kipindi cha miaka mitano ijayo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, Jijini Cairo, Misri.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Jamal Kassim Ali (kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kiarabu (BADEA) Dkt. Sidi Ould Tah, Jijini Cairo, Misri, baada Bednki hiyo kuingia makubaliano na Serikali ya kutoa kiasi cha dola za Marekani bilioni 3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini huku Zanzibar ikitarajia kupkea dola miliuoni 450m katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) na Waziri wa Nchi, Fedha na Mipango-Zanzibar Dkt. Jamal Kassim Ali (kulia) wakiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kiarabu (BADEA) Dkt. Sidi Ould Tah, Jijini Cairo nchini Misri, baada ya Benki hiyo kuahidi kuipatia Tanzania mikopo yenye masharti nafuu pamoja na misaada inayokadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni tatu sawa na shilingi trilioni 7 katika kipindi cha miaka mitano ijayo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, Jijini Cairo, Misri.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ukiwa katika kikao cha majadiliano na uongozi wa juu wa Benki ya Maendeleo ya Kiarabu –BADEA, jijini Cairo nchini Misri, ambapo majadiliano hayo yameweiwezesha Tanzania kutarajia kupata dola za Marekani bilioni 3 (sh. trilioni 7) kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka 5 ijayo.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (mwenye tai ya Bendera ya Taifa) ukiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa juu wa Benki ya Maendeleo ya Kiarabu –BADEA, jijini Cairo nchini Misri, ambapo BADEA itaipatia Tanzania mikopo nafuu na misaada kiasi cha dola za Marekani bilioni 3 (sh. trilioni 7) kwa ajili ya kutekeleza miradi ya mbalimbali ya maendeleo ndani ya kipindi cha miaka 5 ijayo, Jijini Cairo-MIsri. Kutoka kushoto ni Kamishina wa Idara ya Madeni Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Justine Japhet, Mkurugenzi wa Idara ya uendeshaji-Sekta Binafsi wa BADEA Bw. Diab Karrar, kushoto kwa Mhe. Waziri Dkt. Nchemba ni Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Jamal Kassim Ali, Mkurugenzi Mkuu wa BADEA Dkt. Sidi Ould Tah na Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje-Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Robert Mtengule.
(picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
*******************************
Na Benny Mwaipaja, Cairo
BENKI ya Maendeleo ya Kiarabu (BADEA) imeahidi kuipatia Tanzania mikopo yenye masharti nafuu pamoja na misaada inayokadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni tatu sawa na takribani shilingi za Tanzania trilioni 7 katika kipindi cha miaka mitano ijayo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ahadi hiyo imetolewa Jijini Cairo Nchini Misri na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Dkt. Sidi Ould Tah alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
“Tumekuwa na majadiliano ya kina na yenye tija na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania pamoja na ujumbe wake ambapo tumejadili mambo mengi ya msingi kwa ajili ya uhusiano wetu kama Benki na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tuko tayari kutoa fedha hizo” alisema Dkt. Tah.
Alifafanua kuwa fedha hizo zitatolewa katika kipindi cha miaka 5 ya utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo katika maeneo matano ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, elimu, kilimo, kuimarisha sekta binafsi pamoja na kuwajengea uwezo wataalam.
“Tunampongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania kwa ujumla kwa kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa n chi yake na sisi tunaahidi kwamba tutashirikiana naye katika mipango yake ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa Upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba aliishukuru Benki hiyo kwa kuamua kutoa kiasi hicho kikubwa cha fedha ambacho kitasaidia kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka kupitia miradi ya kimkakati waliyokubaliana kupatia fedha hizo.
Alisema kuwa BADEA ni wadau wakubwa wa maendeleo nchini ambapo mpaka sasa wametoa mikopo na misaada inayofikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 2.24 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ukiwemo mradi mkubwa wa maji uanaoanzia Mwanga kwenda Same mkoani Kilimanjaro.
Dkt. Mwigulu alisema kuwa mikopo na misaada ya dola za marekani bilioni 3 zitakazotolewa na Benki hiyo katika kipindi cha miaka 5 ijayo zitatumika kuboresha Nishati, ujenzi wa miradi zaidi ya 14 ya kilimo cha umwagiliaji, ufugaji na ujenzi wa barabara zitakazofungua fursa za kiuchumi kwenye maeneo yanayozalisha bidhaa zikiwemo za kilimo.
“Fedha hizi ambazo BADEA watatupatia zitatumika pia kuendeleza sekta binafsi ambapo benki zitapatiwa sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya kutoa mikopo yenye riba nafuu kwenye sekta za uzalishaji na kukuza ajira kwa vijana na wanawake kupitia shughuli mbalimali ikiwemo biashara na shughuli nyingine za ujasiliamali” alisema Dkt. Nchemba.
Naye Waziri wa Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Jamal Kassim Ali alisema kuwa Zanzibar itanufaika na sehemu ya fedha hizo za mikopo nafuu na misaada ambapo kiasi cha dola za Marekani milioni 450 kitatumika kutekeleza miradi kadhaa ya kimkakati.
Aliitaja baadhi ya miradi ambayo fedha hizo zitaelekezwa kuwa ni Ujenzi wa Uwanja wa Ndege Kisiwani Pemba ukihusisha njia ya kurukia ndege na jengo la abiria, ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni, ujenzi wa vyuo vya ufundi vitano vya VETA pamoja na maghala ya kuhifadhia mafuta.
Dkt. Ali alisema kuwa hatua hiyo itachangia kusisimua zaidi uchumi wa nchi na pia kukuza ajira ambazo ni changamoto kubwa hivi sasa na kuishukuru Benki hiyo ya Maendeleo ya nchi za Kiarabu BADEA kwa uamuzi huo wa kutoa fedha kuchangia maendeleo ya nchi.
0 Comments