Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MULAMULA AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA IRELAND


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiteta jambo na Balozi wa Jamhuri ya Ireland nchini Mhe. Mary O'Neil walipokutana kwa mazungumzo leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Balozi wa Jamhuri ya Ireland nchini Mhe. Mary O'Neil akimuelezea jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) walipokutana kwa mazungumzo leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

.................................................

Na Waandishi wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Ireland nchini Mhe. Mary O’Neil katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha mahusiano ya muda mrefu yaliyopo baina ya Tanzania na Ireland.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri Mulamula ameiomba Serikali ya Ireland kusaidia harakati za Tanzania za kushawishi na kuvutia uwekezaji na biashara nchini ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi na kuleta maendeleo kwa watu wake.

Mhe. Waziri pia ameomba Ireand kuendelea kusaidia eneo la kuwawezesha na kuwajengea uwezo vikundi vya kijamii vya wanawake nchini ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi za ufadhili wa masomo kwa wananchi wa Tanzania.

“Tanzania na Ireland tumekuwa na mahusiano mazuri kwa muda mrefu sasa, mmekuwa mkitusaidia katika maeneo mbalimbali, niombe muelekeze nguvu zenu katika kusaidia vikundi vya kijamii vya wanawake nchini ili kuwasaidia hasa katika kuwajengea uwezo ili nao washiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya nchi yetu,” amesema Waziri Mulamula.

Naye balozi wa Ireland nchini Mhe. O’Neil ameahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na kuongeza kuwa kuna muwekezaji kutoka nchini humo ambaye ameonesha utayari wa kuwekeza katika eneo la ubanguaji wa Korosho mjini Mtwara.

Balozi O’Neil pia amesema nchi yake kupitia taasisi ya utawala wa sheria inashirikiana na Mahakama ya Tanzania kuangalia namna ya kupunguza unyayasaji wa kijinsia katika jamii mbalimbali nchini na wanatarajia kushiriki kikamilifu katika siku 16 za kupinga ukatili huo zinazotarajiwa kufayika nchini.

“Taasisi ya ‘Irish rule of law’ kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania hasa katika eneo la unyanyasaji wa kijinsia zinaangalia kwa pamoja juu ya namna ya kupunguza vitendo hicyo nchini na tutashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya mwaka huu ya siku 16 za kupinga vitendo hivyo,” amesema Balozi O’Neil

Post a Comment

0 Comments