Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ugogoni wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani Kongwa.
Wananchi wa Kijiji cha Ugogoni wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani ya Kongwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Remidius Mwema, akitoa shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa niaba ya wananchi wa Kongwa wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani Kongwa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Chimotolo, Bw. Shadrack Leng’ata akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani Kongwa.
Mratibu wa TASAF Wilaya ya Kongwa, Bw. Elias Chilemu akijibu hoja ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Chimotolo kwa niaba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani Kongwa.
*****************************
Na. Nasra H. Mondwe - Kongwa
Tarehe 11 Novemba, 2021
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka wananchi wa Kongwa kuuona mradi wa TASAF kama neema iliyoshushwa na Serikali ambayo ni fursa itakayowasaidia kuboresha maisha yao.
Mhe. Ndejembi amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ugogoni, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF III) wilayani Kongwa.
Mhe. Ndejembi amewaeleza wananchi hao kuwa, kupitia ruzuku wanayoipata wanaweza kuboresha maisha yao kwa kuibua miradi mbalimbali ikiwemo ufugaji, kilimo pamoja na kuboresha makazi yao.
Mhe. Ndejembi amesema katika kuhakikisha fedha za mradi huo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Serikali, wanufaika wa TASAF wanapaswa kutumia fedha hizo wanazozipata kuboresha maisha yao badala ya kufanya anasa.
“Fedha hizo mnazozipata kupitia TASAF sio za kufanyia anasa bali zinatakiwa zitumike katika masuala ya maendeleo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali ya kuboresha maisha yenu,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Vilevile ameeleza kuwa TASAF ni mradi kama ilivyo miradi mingine, kuna siku utafikia ukomo hivyo walengwa wanapaswa kutumia fursa hiyo kwa ufasaha ili wasijute kwa kutotumia fedha hizo kuboresha maisha yao badala yake waishukuru Serikali kwa kuweza kuwasaidia kutatua changamoto zao kupitia Mradi huo wa Kunusuru Kaya Masikini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Remidius Mwema, amemuahidi Mhe. Ndejembi kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wananchi hao katika kuboresha maisha yao.
Mhe. Mwema amemhakikishia Naibu Waziri huyo kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Mpango huo kwa Vijiji vyote 87 na kata zote ili kuinua uchumi wa walengwa wa Mpango huo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi anaendelea na ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Wilaya ya Kongwa baada ya kumaliza ziara hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.
0 Comments