******************
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe amewataka Wabunge wanawake wa Tanzania kuwa Vinara katika kuelimisha Jamii juu ya urasimishaji wa biashara.
Mhe. Kigahe ameyasema hayo leo Novemba 8, 2021 jijini Dodoma wakati wa mafunzo yaliyotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa Wabunge wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ameeleza kuwa wanawake wanapopata elimu kuhusu njia sahihi za urasimishaji biashara watakuwa walimu wazuri katika vikundi mbalimbali vya wanawake katika maeneo yao.
“Moja ya changamoto kubwa iliyopo ni kwamba shughuli nyingi za ujasiriamali ambazo nyingi zinafanywa na wanawake bado hazijarasimishwa, hazina majina ya biashara wala nembo hivyo wanashindwa kunufaika nazo,” amesema Mhe. Kigahe.
Akizungumza kuhusu dhima kuu ya mafunzo hayo, Mkurugezi wa Leseni kutoka Wakala wa Usajili wa BRELA, Bw. Andrew Mkapa amesema kuwa mafunzo haya ni kuwajengea uwezo Wabunge wanawake kuhusu Urasimishaji wa biashara na Majukumu.
“Tupo katika mafunzo haya kuwajengea uwezo Wabunge wanawake waweze kufahamu taratibu za urasimishaji wa biashara kwa njia ya mtandao ili waweze kuwa vinara katika kuwaelimisha wanawake wengine kuhusu taratibu hizi.”alisema Bw. Mkapa.
Katika mafuzo hayo yaliyohudhuriwa na Wabunge Wanawake 142, elimu iliyotolewa ilihusu Usajili wa Kampuni, Majina ya Biashara, Alama za Biashara na Huduma, Utoaji wa Leseni za Biashara kundi A, Leseni za Viwanda na Hataza.
0 Comments