Ticker

6/recent/ticker-posts

USIYOYAJUA KUHUSU WIZI, UTAPELI KATIKA UCHANGUDOA



 Na JUMA ISSIHAKA

NI mama wa mtoto mmoja, siku zote huamini katika kile anachokifanya kwa kuwa ndiyo humuingizia kipato cha kuendesha maisha yake pamoja na mtoto wake.

Aliponiona aliamini ningekuwa mteja wake, aliniangalia usoni kwa kunichombeza, mavazi yake na mwendo kufika nilipo yaliniaminisha kwamba anafanya biashara ya ngono.

Wakati naduwaa nisijue la kufanya alinishika mkono, akitaka nieleze aina ya huduma nayohitaji na gharama zake.

Nikimuomba mama huyo walau nizungumze nae kidogo, naam alikubali na mazungumzo yetu kuanza eneo ambalo yalimwezesha kunieleza namna anavyofanya biashara hiyo licha ya kuwa imeharamishwa.

Alijitambulisha kwa jina moja la Silvia akaanza kunieleza kuwa yeye ni mama wa mtoto mmoja na anajiingizia kipato kwa kuuza mwili yaani biashara ya ngono mkoani Arusha.

Wengi huwatambua kwa jina la makahaba yote hii ni kuonyesha uharamu wa biashara yao na namna jamii isivyokubaliana na matendo na kazi zao.

Tuwaonapo tunadhani wanafanya biashara rahisi lakini utekelezwaji wake umegubikwa na changamoto lukuki, huku vitendo vya wizi na utapeli vikitajwa kushamiri na kuifanya kuwa hatari zaidi kwa wateja wake.

Sylvia anasema tangu ameanza kuifanya biashara hiyo hadi sasa ni mwaka mmoja na miezi mitano na amesukumwa na hali ngumu ya maisha aliyokumbana nayo.

“Mimi sikusoma, nipe mchongo basi nitaacha kufanya hivi…. Unafikiri mimi napenda?” alihoji.



WIZI NA BIASHARA YA NGONO

Sylvia anabainisha, si ajabu kwa mteja wa ngono kuibiwa au kutapeliwa kinachoangaliwa ni maslahi ya siku husika, hakuna wema wala aibu wakati wa utekelezwaji wa yote hayo.

Ingawa kuna aina hiyo ya matukio, Sylvia anasema wapo baadhi ya wanawake wanaouza miili yao wanaofanya shughuli hiyo kwa uaminifu, lakini mwenendo wa tabia za wengi hufanya wote wasiaminiwe.

Anataja moja ya silaha kubwa inayofanikisha wizi kwa wateja wanaoonyesha kuwa na fedha ni dawa za kulevya wanazoweka katika matiti kisha kumlaghai mwanaume ayanyonye au kuyalamba.

Anabainisha si kawaida kwao kumwachia mteja maziwa ayachezee au kufanya lolote, mara nyingi huyaziba kwa brazia na kuruhusu maeneo mengine ya mwili yatumiwe.

“Unaficha matiti kwa makapuku ‘wasio na pesa’ ukiona mteja ana hela na amekuja nazo au ana vitu vya thamani unamwachia anyone ili alewe unachukua mzigo unasepa… atanionea wapi mimi,” anafafanua.

Ili kutekeleza wizi huo mara nyingi, anasema wanakuwa wameelewana na wahudumu wa nyumba za kulala wageni au Hoteli wanazofikia na wateja, baada ya kufanikisha huwagawia sehemu ya walichoiba.

“Mwanamke anayefanya biashara ya ngono akikataa kuvua brazia na kukunyima usichezee maziwa yake usimlazimishe maana ni kwa usalama wako ...anacheka.... utaibiwa,” anaongeza huku akiangua kicheko kwa mara nyingine.

Sylvia anasema, ili kupunguza nguvu ya mteja kushiriki tendo kwa muda mrefu ambayo inawachelewesha kutafuta wateja wengine, katika kinga ‘kondomu ’ huweka dawa ya kudhoofisha uwezo wa mwanaume.

Hata hivyo anabainisha sababu za changudoa kumvalisha mteja kinga si sehemu ya kuboresha huduma, bali ni mbinu ya kupima maumbile ya mwanaume kama atamudu kushiriki nae tendo ama laa.

Anasema akibaini mwanaume ana maumbile makubwa kiasi cha kushindwa kuhimili, yupo tayari kuacha fedha na kwenda kutafuta mteja mwingine, kwa kuwa maumivu atakayosababishiwa huenda yakamfanya ashindwe kuendelea na biashara kwa siku hiyo.

Anataja mbinu nyingine wanazozitumia kufanya shughuli hiyo ni matumizi ya kinga, ambapo kwao huitumia kwa faida tatu kibiashara.

Anasema faida ya kwanza ni kujikinga dhidi ya magonjwa ya ngono, pili ni kujikinga na ujauzito na tatu haichoshi hivyo huwafanya kumudu kushiriki tendo na wanaume wengi.

“Ukifanya bila kondomu utachubuka mapema utapata maumivu, kwahiyo katika mazingira yasiyo na kinga tunatumia mafuta lainishi ambayo yenye hayasababishi michubuko,” anabainisha.

Anaeleza kwa siku hukusanya kati ya sh. 100,000 hadi 120,000 kikiwa ndiyo kima cha mwisho alichojipangia kukusanya kwa siku kisha anakwenda kulala, japokuwa zipo baadhi ya siku kinapungua.

Anaweka wazi kwamba ni mwaka na miezi mitano sasa tangu aanze biashara hiyo, mwanzo uligubikwa na changamoto nyingi yakiwemo maumivu kutokana na kutokuwa na uzoefu wa shughuli hiyo.

Anasema kuwa mjamzito hakuathiri chochote katika biashara hiyo kwani, wapo baadhi ya wateja wanaopenda wajawazito, hata yeye alifanya hadi alipokaribia kujifungua.

Kwa mujibu wa Sylvia, ni ngumu kwa changudoa kuruhusu kwenda eneo asilolitambua na badala yake huchagua maeneo wenye uzoefu nayo pekee ili wawe na nafasi ya kufanya mambo mbalimbali uki utapeli.

Hata hivyo, anaeleza ni ngumu kwa yeyote aliyeingia kwenye shughuli hiyo kuachana nayo kwa kuwa, tayari anajiona hana utu na thamani tena mbele ya jamii.

Anasimulia wengi huingia katika biashara ya ngono baada ya kukumbwa na changamoto zilizowafanya kukosa fikra mbadala.

Anaeleza binafsi alifikiria kuacha kufanya shughuli hiyo, lakini amejiwekea lengo la kufanikisha hilo baada ya kukamilisha ujenzi wa nyumba yake.

Kwa mujibu wa Sylvia, changudoa hapati hisia zozote wakati wa tendo na mteja wake na badala yake anaishia kufanya kama kazi ya kujiongezea kipato.

Anabainisha kwamba pamoja na shughuli hiyo kutokuwa halali na wakati mwingine kukamatwa na Vyombo vya Ulinzi na Usalama lakini wapo baadhi ya watumishi hao ni wateja wao.

Mhudumu Gesti asimulia magumu anayopitia Hassan Hassan ni mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Monjes jijini Arusha, eneo ambalo Changudoa hukaa kusubiri wateja na wakati mwingine huikodi kwa ajili ya shughuli zao, anasema ni mwaka wa tano sasa tangu anafanya kazi eneo hilo.

Anaeleza ukaribu na urafiki wake na wanawake hao umemuathiri kiasi kwamba hapati hisia za haraka hata anapokuwa na mkewe.

“Wakati wote nakuwa na hawa wanawake hapa karibu. Nimekuwa rafiki yao kwa sasa, unajua mavazi wanayovaa na wakati mwingine wananifanyia makusudi kwahiyo kwa sasa nakosa hisia hata nikiwa na mke wangu,” anasema.

Anasema kwa sasa amewazoea hivyo hateseki tena na mavazi, ukilinganisha na wakati anaanza kufanya kazi hiyo.

Anafafanua kwamba wakati mwingine wanamtumia kama dalali wa kuwatafutia wateja, kwa kuwa wanamuamini akiwapigia simu kuwapa taarifa za mteja kutoka eneo lolote jijini humo, wanakwenda kutoa huduma.

UCHANGUDOA NA DAWA ZA KULEVYA

Hassan anasema kutokana na uzoefu wake, wanawake wote aliowahi kuwaona wakifanya shughuli hiyo wakiwemo marafiki zake, wengi wamekuwa wakitumia dawa za kulevya.

“Kama hali kijiti ‘Bangi’ basi atakuwa anakula unga au kilevi chochote, lakini zaidi ni walevi wa pombe,” anasema.

DAKTARI AFUNGUKA

Akizungumzia hatua ya kufanya biashara hiyo wakati wa ujauzito, Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Profesa Andrea Pembe, anasema ni hatari kwa mtoto iwapo tendo litafanyika bila kinga.

Anafafanua kwamba mjamzito atakaposhiriki tendo hilo bila kutumia kinga huenda akaambukiza magonjwa ya ngono na hivyo kumuathiri na mtoto.

Anaeleza hatari nyingine ni kwa mjamzito mwenye mimba inayotishia kutoka.

“Kama mjamzito ana mimba inayotishia kutoka ni hatari kushiriki tendo kwa sababu manii ya mwanaume yakimgusa mtoto huongeza homoni na kusababisha kuzaa mtoto kabla ya muda wake, hivyo anaweza kuzaa njiti,” anasema.

Post a Comment

0 Comments