Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akisoma hotuba wakati akifungua rasmi Tamasha la mvinyo Dodoma Wine Festival Katika Viwanja vya Mashujaa Jijini Dodoma, tamasha lililofanyika kwa lengo la kuhamasisha na kutangaza zao la zabibu na bidhaa zake.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akipata maelezo ya Mvinyo kutoka kwa Elias Mtiwabi Mkulima na Msindikaji wa Zabibu wa Wilaya ya Bahi (katikati) ni Afisa Ushirika Ndimolwo Laizer akifuatilia maelezo.
Bw. Elias Mtwabi Mkulima wa zabibu na msindikaji wa mvinyo wa zabibu kutoka Wilaya ya Bahi akitoa elimu kwa wadau mbalimbali waliofika katika Tamasha la mvinyo jinsi usindikaji wa zabibu unavyofanyika.
Baadhi ya washiriki wakimsikiliza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati akifungua rasmi Tamasha la mvinyo Dodoma Wine Festival Katika Viwanja vya Mashujaa Jijini Dodoma, tamasha lililofanyika kwa lengo la kuhamasisha na kutangaza zao la zabibu na bidhaa zake.
............................................................................
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali inafanya jitihada kuboresha na kuendeleza zao la zabibu kwa kuanzisha na kuendeleza Vyama vya Ushirika wa zabibu ili kuongeza fursa za masoko na tija kwa wakulima wa zabibu nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Mvinyo Dodoma Wine Festival katika Viwanja vya Mashujaa Jijini Dodoma Novemba 5, 2021 amebainisha baadhi ya hatua mbalimbali zinazoendelea kutekelezwa na Serikali katika kuhakikisha zao la zabibu linaimarika miongoni mwa mazao ya kimkakati.
Hatua hizo ikiwa ni Pamoja na wakulima wa zabibu kujikusanya Pamoja na kuanzisha vyama vya ushirika ili Serikali iweze kuwafikia kwa urahisi kwaajili ya huduma mbalimbali za kilimo pamoja na utafutaji wa masoko. Waziri Mkuu pia ameanisha kuwa mahitaji ya miche ya zabibu kwa wakulima ni laki tatu wakati uzalishaji ni laki moja. Hivyo, amevitaka vyama vya Ushirika kuanza kuzalisha miche hiyo kwaajili ya wakulima wa vyama hivyo.
“Tunaanzisha Vyama vya Ushirika ili iwe rahisi kupata huduma za ugani, mikopo na vyama hivi vihimizwe kuzalisha miche ya zabibu ili wakulima waweze kupata huduma ya miche bora kutoka kwenye vyama itakayosaidia kuongeza uzalishaji,” alisema Waziri Mkuu
Aidha, Waziri Mkuu amewataka wananchi wengi kuchangamkia fursa ya kilimo cha zabibu kwani bado uzalishaji ni mdogo huku akitaja kuwa Mkoa wa Dodoma una jumla ya eka Milioni 2.1 zinazofaa kwa kilimo na uwekezaji wa zabibu ambao ni fursa ya kujikwamua kiuchumi.
Hatua nyingine alizozibainisha kuendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuendeleza zao la zabibu ni Pamoja na kuimarisha tafiti ya zao hilo, upatikanaji wa mbegu bora, kuongeza upatikanaji wa huduma za ugani, kuhamasisha viwanda vya usindikaji wa zabibu, usajili wa wakulima wa zabibu, kusimamia na kufufua vyama vya Ushirika wa zabibu sambamba na kuweka miundombinu ya umeme kwenye miradi ya mashamba ya zabibu.
Akielezea malengo ya Tamasha la Mvinyo Jijini Dodoma Bi. Atitwe Makweta mratibu wa tamasha hilo amesema, tamasha hilo ni la nne kufanyika mkoani Dodoma likilenga katika kuhamasisha zao la zabibu na bidhaa zake ili kuongeza tija ya mnyororo wa thamani ya uzalishaji zabibu. Akiongeza kuwa mwaka huu Kauli Mbiu ya Tamasha hiyo ni “Onja Kila Siku pata ladha tofauti”
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Antony Mavunde ameshukuru wadau wa zao la zabibu kwa kuitika wito wa kushiriki tamasha hilo huku akiiomba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuendelea kusaidia wakulima katika upatikanaji wa masoko, uhifadhi mzuri wa zabibu pamoja na masuala ya utaalamu wa Kilimo cha zabibu ili kuongeza thamani ya mnyororo wa zabibu utakaochangia kuongeza uchumi na pato la Taifa.
0 Comments