Mkuu wa Wilaya ya Kiteto ndugu Mbaraka Alhaji Batenga akifungua mafunzo ya udhibiti wa sumukuvu kwa wafanyabiashara, wasafirishaji na wasindikaji wa mahindi na karanga. Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa TBS Bw.Jabir Abdi akiongea na washiriki wa mafunzo kwa wafanyabiashara, wasafirishaji na wasindikaji wa mahindi na karanga wilayani Kiteto. Baadhi ya washiriki wa mafunzo kwa wafanyabiashara, wasafirishaji na wasindikaji wa mahindi na karanga na bidhaa zake katika wilaya ya kiteto.
******************
Serikali chini ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) imeanza rasmi kutoa mafunzo kupitia Mradi wa Kitaifa wa Kudhibiti Sumukuvu "Tanzania Initiative for Preventing Aflatoxin Contamination - TANIPAC" yanayotarajiwa kutolewa katika wilaya 18 zilizopo kwenye mikoa 10 nchini. Mafunzo ya mradi huo yalizinduliwa rasmi jana wilayani Kiteto mkoani Manyara na kuhudhuriwa na washiriki 120, ambapo mradi huo upo chini ya Wizara ya Kilimo na TBS imekabidhiwa jukumu la kutoa mafunzo hayo.
Akizungumzia na waandishi wa habari wilayani hapa kuhusu wilaya na mikoa itakayonufaika na mafunzo hayo Bw.Jabir Abdi wa TBS alitaja wilaya hizo kuwa ni za Kondoa, Chemba, Bahi, Kongwa, Babati, na Kiteto.
Wilaya zingine ni Namtumbo,Newala, Nanyumbu, Nzega, Urambo, Kibondo, Kasulu, Buchosa, Bukombe, Itilima, Kilosa na Gairo. Kuhusu mikoa zilizopo wilaya hizo, Abdi alisema ni Dodoma, Manyara, Ruvuma, Mtwara, Tabora, Kigoma, Mwanza, Geita, Simiyu na Morogoro.
Tafiti za awali za mradi huu zimebaini maeneo hayo tajwa kuwa kuna changamoto ya uwepo wa sumukuvu katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mahindi na karanga na bidhaa zake.
Abdi aliwataja walengwa wa mafunzo hayo kuwa ni wafanyabiashara, wasafirishaji na wasindikaji wa mahindi na karanga pamoja na bidhaa zake.
Abdi alitaja faida za mafunzo kuwa yalenga kulinda afya za binadamu, kuwezesha biashara ya mazao ya mahindi na karanga, kulinda afya za mifugo na kuwezesha utoshelevu wa chakula salama.
Alitaja faida nyingine kuwa kuhimili ushindani katika masoko ya ndani, kikanda na nje ya nchi.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo jana Mkuu wa Wilaya ya Kiteto ndugu Mbaraka Alhaji Batenga, alipongeza uamuzi wa Serikali kuanzisha mafunzo hayo, kwa sababu chakula ni hitaji muhimu sana kwa binadamu na ustawi wa maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Hata hivyo, alisema usalama wa chakula unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchafuzi wa sumukuvu ambao husababisha madhara ya kiafya na hata kiuchumi.
Batenga, alisema sumukuvu huathiri zaidi mazao ya mahindi na karanga ambayo ni sehemu muhimu ya chakula cha Watanzania hapa nchini. "Kwa sababu hiyo sisi sote tunatakiwa kuzingatia mikakati ya kukabiliana na sumukuvu ili vyakula vyetu viendelee kuwa salama kwa muda wote," alisisitiza Batenga.
Alifafanua kwamba anatambua nafasi ya wafanyabiashara, wasindikaji na wasafirishaji kwa ujumla wao na mchango wao walionao, hivyo serikaii imeandaa mafunzo hayo mahususi kwa ajili yao ili kuwajengea uwezo kwa ajili ya udhibiti sumukuvu.
Alisema umuhimu huu unasabishia suala la usalama wa chakula kupewa kipaumbele katika kulinda afya, jamii na uchumi wa nchi, kwa kuwa kigezo muhimu cha biashara kitaifa na kimataifa, kwani chakula kisicho salama husababisha madhara ya kiafya na vifo kwa walaji pamoja na athari za kiuchumi.
Alihimiza wadau hao kuzingatia mambo muhimu yanayoshauriwa na wataalam ili kudhibiti sumukuvu katika chakula, ikiwa ni pamoja na kuzingatia kanuni bora za kilimo kama inavyoshauriwa na wataalam, kuvuna na kuondoa shambani mahindi na karanga mara baada ya kukomaa vizuri na kukaushia vizuri mazao yaliyovunwa kabla kuhifadhi.
Nyingine ni kuepuka kurundika mazao moja kwa moja kwenye sakafu, kuhakikisha wanahifadhi vizuri mazao na kwa lengo la kuepuka wadudu waharibifu, wanyama, joto kali na unyevunyevu.
0 Comments