Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA NA RWANDA KUIMARISHA USHIRIKIANO BAINA YA WAFANYABIASHARA ZA KITALII


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) na Naibu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, Zephanie Niyonkuru wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Utalii uliofanyika katika hoteli ya Kigali Serena nchini Rwanda leo.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Wiki ya Utalii ya Rwanda kwenye hoteli ya Kigali Serena nchini Rwanda leo.


Naibu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, Zephanie Niyonkuru ambaye pia ni mgeni rasmi katika uzinduzi wa Wiki ya Utalii akifungua maadhimisho hayo yanayoendelea katika hoteli ya Kigali Serena nchini Rwanda leo.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) na Naibu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, Zephanie Niyonkuru wakimsikiliza Afisa Utalii Mwandamizi kutoka TAWA, Stephen Madenge akitoa ufafanuzi kuhusu vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini Tanzania katika Wiki ya Utalii ya Rwanda inayoendelea katika hoteli ya Kigali Serena nchini Rwanda.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (katikati), Naibu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, Zephanie Niyonkuru (kushoto) na Mwenyekiti wa Idara ya Utalii ya Rwanda, Aimable Rutagarama wakifuatilia matukio ya Wiki ya Utalii katika hoteli ya Kigali Serena nchini Rwanda leo.

*************************

Na Happiness Shayo - Rwanda

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Rwanda imekubaliana kuwaunganisha wafanyabiashara wa Sekta ya Utalii wa nchi hizo ili kukuza utalii.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) katika Maadhimisho ya Wiki ya Utalii ya Rwanda yanayoendelea nchini humo.

“Kikubwa tumeweza kukutana na Rais wa wafanyabiashara za kitalii wa hapa nchini Rwanda na tumeomba wafanyabiashara wa huku kushirikiana na wa kwetu kukuza Sekta ya Utalii” amesema Mhe. Masanja.

Aidha, Mhe. Masanja amewataka Watanzania kuwa wazalendo kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko nchini mwao.

“ Nawaomba Watanzania kwa umoja wetu tuendelee kuwa wazalendo, tuipende nchi yetu na tuendelee kuitangaza nchi yetu kama ambavyo wenzetu wa Rwanda wanavyofanya” Mhe. Masanja amesisitiza.

Naye, Naibu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, Zephanie Niyonkuru amesema kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Utalii ya Rwanda yamelenga katika kuibua ubunifu katika Sekta ya Utalii nchini humo na kutoa tuzo kwa mshindi.

Ameongeza kuwa pia maonesho hayo yanatoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani na wa Kimataifa kuuza bidhaa na huduma zao kwa wadau wengi kutoka Bara la Afrika.

Kwa upande wake Afisa Masoko Mkuu kutoka Bodi ya Utalii Tanzania, Bernard Mtatiro amesema kupitia Wiki ya Utalii ya Rwanda Tanzania itapata fursa ya kutangaza mazao mapya ya utalii kwa nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tumejipanga kutangaza mazao mapya ya utalii kwa mfano Utalii wa Mchezo wa gofu, reli ya mwendokasi (SGR), Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere” amefafanua Bw. Mtatiro.

Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ya “Kujenga Upya Utalii kwa Ukuaji Endelevu”yamehudhuriwa na washiriki kutoka nchi za Tanzania, Ghana, Botswana Kenya, Nigeria, Kongo, Afika Kusini, Somalia, Zimbwabwe pamoja na wadau wa utalii kutoka Dubai.

Post a Comment

0 Comments