Mkurugenzi Mkuu wa Burundi Lea Ngabire (kushoto) akizungumza kwenye kikao na Menejimenti ya Shirika la Posta nchini katika Makao Makuu ya Shirika hilo, mara baada ya ziara yake katika Ofisi za Posta Kuu Dar es Salaam. Kulia ni Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Daniel Mbodo
Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Daniel Mbodo akizungumza wakati wa kikao cha Menejimenti ya Shirika hilo na ugeni kutoka Burundi, katika Makao Makuu ya Shirika hilo, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Burundi Bi. Lea Ngabire
Mkurugenzi Mkuu wa Burundi Bi. Lea Ngabire (wa pili kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Afisa mwandamizi wa Shirika la Posta nchini Bi. Ledegunda Tarimo (kushoto) kuhusiana na namna ambavyo Shirika la Posta Tanzania linaendesha shughuli zake katika kuhudumia wananchi. Kulia ni Meneja Biashara Barua na usafirishaji Jasson Kalile.
Mkurugenzi Mkuu wa Burundi Bi. Lea Ngabire (kushoto) akikabidhi zawadi kwa Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Daniel Mbodo (kulia), mara baada ya kikao hicho
Mkurugenzi Mkuu wa Burundi Bi. Lea Ngabire (kushoto) akikabidhi zawadi kwa Kaimu Meneja Mkuu Uendeshaji Biashara Constantine Kasese (kulia) mara baada ya kikao hicho. Anayetazama katikati ni Kaimu Postamasta Mkuu Bw. Macrice Daniel Mbodo
Mkurugenzi Mkuu wa Burundi Bi. Lea Ngabire (kushoto) akikabidhi zawadi kwa Kaimu Meneja Mkuu Rasilimali za Shirika la Posta Aron Samwel (kulia) mara baada ya kikao hicho. Anayetazama katikati ni Kaimu Postamasta Mkuu Bw. Macrice Daniel Mbodo
Afisa masoko mwandamizi wa Shirika la Posta Tanzania Rose Mafuru akiwaonesha Maafisa waandamizi wa Shirika la Posta Burundi namna ambavyo Shirika la Posta nchini linafunga mizigo ya wateja kwa ajili ya kusafirisha sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi
Mkurugenzi Mkuu wa Burundi Bi. Lea Ngabire (aliyekaa kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa Shirika la Posta Tanzania. Aliyekaa kulia ni Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta nchini Macrice Daniel Mbodo
.......................................................................
SHIRIKA la Posta Tanzania limepokea ujumbe wa viongozi waandamizi kutoka Shirika la Posta la Burundi (RNP).
Ujumbe wa Posta ya Burundi umeongozwa na Mkurugenzi Mkuu Bi. Lea Ngabire akiambatana na Bwana Oliver Ndaishimye kutoka Kitengo cha IT na Bwana Deo Musirabi Kutoka idara ya uendeshaji wa barua.
Ujumbe wa Posta Burundi umekuja Posta Tanzania ukiwa na lengo la kubadilishana uzoefu hususan kwenye eneo la uendeshaji wa huduma za Posta kidijitali ambako Shirika la Posta Tanzania kwa sasa limejidhatiti kidijitali
Akizungumza wakati wa kukaribisha ugeni huo, Kaimu Postamasta Mkuu Bwana Macrice Mbodo amesema ugeni huu ulioongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Posta Burundi ni ujio wenye faraja kwa Tanzania hususan Shirika la Posta Tanzania ikizingatiwa mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi hizi mbili, si tu kuwa ni marafiki bali ni ndugu.
"Kama mnavyofahamu hivi karibuni Rais wa Burundi Mhe. Evariste Ndaishimiye alitembelea Tanzania na kukutana na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa ngazi ya kitaifa, leo na sisi Mashirika ya Posta tumefuata nyayo za viongozi wetu wakuu ndiyo maana unaona Posta ya Burundi na uongozi mzito upo hapa kwetu kwenye ziara ya kikazi na kubadilishana ujuzi" alisema Bwana Mbodo.
Kaimu Postamasta Mkuu aliongeza kuwa, maboresho ya kiutendaji pamoja na mifumo ya uendeshwaji wa Shirika la Posta nchini yamekuwa kivutio kwa nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) hadi kupelekea nchi nyingi kutaka kutembelea na kujifunza kutoka Posta ya Tanzania
Ikumbukwe kuwa, Tanzania iliweza kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania duniani kupitia Shirika la Posta Tanzania kufuatia kushinda nafasi mbili kwa Tanzania kuwa mjumbe wa Baraza la Utawala na Baraza la Uendeshaji wa Umoja wa Posta Duniani katika chaguzi zilizofanyika katika Mkutano Mkuu wa 27 wa Umoja wa Posta Duniani nchini Ivory Coast mwezi Agosti, 2021.
Sambamba na hilo Tanzania iliaminiwa kuongoza Kamati nyeti na muhimu ya Huduma za Posta na Biashara Mtandao (Physical Services and E-Commerce) ikiwa ni Mwenyekiti mwenza pamoja na Uswisi, nchi yenye mafanikio makubwa kwa utoaji wa huduma zenye ubora kabisa zinazoendana na teknolojia za kisasa za kiposta Duniani.
Bwana Mbodo amefafanua kuwa Tanzania ni mwenyeji wa Umoja wa Posta Barani Afrika, Makao Makuu yake yakiwa jijini Arusha, Kama ilivyo Uswisi ni nchi mwenyeji wa Umoja wa Posta Duniani, Makao yake Makuu yakiwa kwenye mji wa Berne na posta yao ni ya mfano Duniani, tunataka pia Posta Tanzania iwe Posta ya mfano Barani Afrika na nchi mbalimbali za Afrika zije kujifunza uendeshaji wa huduma za posta za kidijitali ndani ya Shirika la Posta Tanzania.
"Huu ndiyo mwelekeo wetu na tungependa wananchi wayajue haya na waendelee kutuunga mkono tunapotekeleza azma ya kiongozi wetu wa awamu ya sita Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ameifungua nchi kimataifa ili kuleta uwekezaji wa kiuchumi kwa ustawi wa watanzania.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu Bi. Lea Ngabire ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Posta nchini kwa kupokea ujio wao na kukubali kubadilishana uzoefu kwa kuwafundisha mbinu na namna mbalimbali za kuendesha mifumo ya kiposta katika kutoa huduma bora kwa wananchi. Pia Bi. Lea amekiri kujifunza vya kutosha kutoka Shirika la Posta nchini na kuahidi kuutumia ujuzi huo kuboresha huduma za kiposta nchini Burundi
Katika hatua nyingine, Bi. Lea amekabidhi zawadi kwa baadhi ya viongozi wa Shirika la Posta Tanzania kama ishara ya kuendeleza mahusiano na mashirikiano mazuri ya Taasisi hizi mbili
0 Comments