***********************
Na WAMJW-DSM
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatarajia kupokea kiasi cha shilingi Bilioni 437 kwa kipindi cha miaka 5 kwaajili ya miradi ya Afya inayolenga kuwafikia wananchi katika ngazi ya jamii.
Hayo yamesemwa leo 15 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima katika kikao na Mtendaji mkazi wa Shirika lisilo la Kiserikali la USAID Bi. V. Kate Simvongsiri aliyeambatana na Wataalamu kutoka shirika hilo.
Dkt. Gwajima amesema, Shirika hilo linatarajia kutoa kiasi hicho kitachoanza kutumika mwaka kesho, ili kuboresha huduma za afya katika ngazi ya jamii, katika maeneo ya kuimarisha mifumo ya afya, huku akisisitiza mradi huu ni mwendelezo wa mradi wa Boresha afya unaotarajia kumalizika Disemba 31.
"Serikali ya Marekani inatarajia kutoa kiasi cha shilingi Bilion 437 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka kesho, fedha hizo zitatumika katika kuboresha utoaji wa huduma za afya ikiwemo kuimarisha mifumo ya afya katika ngazi ya jamii " Amesema Dkt Gwajima.
Aidha, Dkt. Gwajima ameishukuru Shirika la USAID kwa kuwekeza zaidi ya Dola za kimarekani Bilioni 7.5 kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita, ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 4.9 ziliwekezwa katika Sekta ya Afya ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Aliendelea kusema kuwa, katika kuboresha utoaji huduma kwa wananchi, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeweka vipaumbele katika kuwahudumia wananchi vikiwemo kuendelea kuimarisha miundombinu ya huduma za afya katika ngazi zote, kupunguza vifo vya mama na mtoto vinavyozuilika, ushirikiano katika uanzishwaji wa viwanda vya bidhaa za dawa ikiwemo Chanjo ya UVIKO-19.
Dkt. Gwajima ameendelea kusema kuwa, Serikali imepiga hatua katika mapambano dhidi ya UVIKO-19, kwa kuongeza kasi ya kuwakinga wananchi kupitia afua ya chanjo kupitia kampeni shirikishi na harakishi ya UVIKO-19 iliyoonesha matokeo chanya kwa njia ya elimu kwa jamii.
Mbali nahayo Dkt. Gwajima ameishukuru Serikali ya Marekani kuisaidia Tanzania Chanjo zaidi ya 1,000,000 za Jenssen iliyosaidia kuwakinga wananchi dhidi ya UVIKO-19, huku akiweka wazi kuwa tayari Serikali ya hiyo ya Marekani imeshatoa chanjo nyingine 500,000 za Pfizer zinazotarajia kuwasili Novemba 21.
Pia, Dkt. Gwajima ameliomba Shirika hilo kuendelea kuisaidia Serikali katika mapambano dhidi ya UVIKO-19 ,hususan katika awamu ya pili ya utekelezaji wa awamu ya pili ya mpango Shirikishi na Harakishi wa jamii ili kuendelea kuikinga jamii dhidi ya UVIKO-19.
Nae, Mtendaji mkazi wa Shirika lisilo la Kiserikali la USAID Bi. V. Kate Simvongsiri amesema, tayari Serikali ya Marekani imeongeza chanjo 165,000 za Jenssen ili kuendelea kuwakinga Watanzania zilizoingia tangu Novemba 13, ikiwa ni mkakati wa Serikali hiyo katika kupambana dhidi ya UVIKO-19.
"Serikali ya Marekani imejipanga katika kuhakikisha inatokomeza ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kuleta chanjo 165,000 za Jenssen ambazo tayari zimefika nchini tangu Novemba 13" Amesema.
Aliongeza kuwa, licha ya mapambano dhidi ya UVIKO-19, Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kupambana dhidi ya magonjwa mengine ikiwemo ugonjwa wa UKIMWI na Malaria.
0 Comments