................................
Na WAMJW — Muheza, Tanga.
Serikali imeahidi kuendelea kuboresha huduma za afya Wilayani Muheza, Tanga kwa kuongeza miundombinu ya kutolea huduma za afya na kuendelea kuleta watumishi wa kada za afya wilayani humo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel mara baada ya kufanya ziara katika Wilaya hiyo na kuona hali ya utoaji huduma.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inawajali wananchi wake na itaendelea kuleta miradi ya maendeleo Sekta ya Afya na kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma za afya Muheza” amesema Dkt. Mollel.
Dkt. Mollel amesema Serikali imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Muheza inayoitwa Hospitali ya Samia Suluhu Hassan ambayo imeshaanza kutoa huduma katika majengo saba yaliyojengwa na kukamilika kwa asilimia 100. “Mwaka wa fedha 2020/21 Serikali imetoa kiasi cha Shilingi 500,000,000/= kwa ajili ya kujenga majengo 3 kwa ajili ya wodi ya watoto, wodi ya wanawake pamoja na wodi ya wanaume na majengo hayo yamefikia hatua ya umaliziaji” amesema Dkt. Mollel.
Kwa sasa huduma za matibabu kwa wagonjwa nje zimeshaanza kutolewa katika Hospitali ya Samia Suluhu Hassan huku Dkt Mollel akiahidi kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja Utumishi wataendelea kufanya juhudi za kuleta watumishi Wilayani humo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Godwin Mollel Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa rai kwa watumishi wa Kada za Afya kupata chanjo ya UVIKO-19 ili kujikinga dhidi ya ugonjwa huo na kuwa katika mazingira hatarishi ya kuambukizwa UVIKO-19.
“Watumishi wa Sekta ya Afya wako mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya UVIKO-19 ni vyema kwa wao kupata chanjo yaa UVIKO-19 ili kujikinga na ugonjwa huo” amesema Dkt Mollel.
Aidha Dkt. Mollel amewashukuru watumishi wote wa kada za afya kwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya UVIKO-19 na kuokoa maisha ya watu.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Muheza Mhe. Hamis Mwinjuma amemshukuru Dkt. Mollel kwa kuweza kufika katika Wilaya hiyo kujionea hali ya utoaji huduma za afya huku akitumia nafasi hiyo kuendelea kuiomba Serikali kutoa kipaumbele zaidi Wilayani humo kwakuwa ina uhaba mkubwa wa vituo vya kutolea huduma za afya.
“Wilaya ya Muheza ina Kata 37 ambazo zinahudumiwa na vituo vine tuu vya afya ambavyo vya Serikali ni 2 huku 2 vingine ni vya binafsi, kwa hiyo unaoa ni jinsi gani bado tuna uhitaji wa kuongezewa vituo vya afya Muheza” amesema Mhe. Mwinjuma.
Mhe. Mwinjuma hakusita kutoa shukrani zake za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha Shilingi 250,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kwafungo pamoja na Shilingi 147,389,865/= kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati 3 za Kwakopwe, Kilongo na Pangamila ambazo zahanato zote ujenzi upo katika hatua ya umaliziaji.
0 Comments