Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akihitimisha hafla ya uzinduzi wa Mkakati wa kutokomeza ukeketaji nchini iliyofanyika Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizindua Mkakati wa Taifa wa kutokomeza Ukeketaji nchini katika hafla iliyofanyika Jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa hafla ya uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa kutokomeza ukeketaji wakifuatilia hotuba ya mgeni Rasmi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akisalimiana na baadhi ya Viongozi wa Kimila na Machifu kabla ya kuhitimisha hafla ya uzinduzi wa mkakati wa kutokomeza Ukeketaji nchini iliyofanyika jijini Dodoma.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WAMJW
***********************
Na Mwandishi Wetu Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amekemea vikali vitendo vya ukeketeji kwa watoto kike na kuwataka wanaojihusisha na ukatili huo kuacha mara moja.
Ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akihitimisha hafla ya uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa kutokomeza ukeketaji nchini na kuwataka Wadau wote kuendelea kupambana katika kutokomeza ukeketaji na kuongeza kuwa, Serikali inatambua Mchango wao katika kuwakomboa Mabinti waishio katika mila hizo zilizopitwa na wakati.
“Ukeketaji si jambo zuri na linawakosesha mabinti fursa kwani wanashindwa kujiamini kabisa,vitendo hivyo ni dhambi na havipo kwenye vitabu vya dini na pia ni uonevu wa hali ya juu hivyo Jamii iachane na vitendo hivo”.
alisema Naibu Waziri Mwanaidi
Aidha Mhe. Mwanaidi amewahimiza wadau kutochoka na kuendelea kupambana vikali dhidi ya vitendo vya ukeketaji ili kuwaepusha Watoto wa kike kufanyiwa vitendo hivyo visivyofaa katika jamii.
Awali akizingumza katika uzinduzi wa Mkakati huo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu amesema Mila na Desturi za kuwaanda watoto wa kike kuelekea utu uzima zinaweza kufanyika kwenye Jamii bila kufanya Ukeketaji.
"Kuna mambo ambayo ni mazuri ya kuwaanda vijana lakini kitendo kisichofaa ni ukeketaji, tunayo kazi kubwa ya kufanya ambayo ni kubadili fikra za jamii na ikiwezekana kutafuta namna mbadala ya kuendeleza Mila na Desturi zetu,"
Akiwasilisha Mpango kazi wa kutekeleza Mkakati huo kwa Wadau walioshiriki uzinduzi, Meneja Mradi wa kutoa elimu kuhusu Ukeketaji na afya ya uzazi wa Shirika la AMREF HEALTH AFRICA, Dkt. Jane Semfano amesema vitendo vya Ukeketaji nchini vimepungua huku akionesha takwimu za 1996 ilikuwa ni asilimia 18 na utafiti wa mwaka 2015/16 ulionesha kwamba msichana mmoja kati ya 10 ndiyo amekeketwa.
Mmoja wa Mangariba aliyestaafu kazi hiyo kutoka Mkoa wa Singida Hawa Hussein amesema kitendo hicho ni hatari kubwa kwa sababu ameshuhudia madhara mengi ikiwemo vifo kupitia mikononi mwake hivyo amewaasa Mangariba wote kuacha vitendo hivyo.
"Ninawasaidia wamama wengi kujifungua zaidi ya 200 pamoja na kuwapa elimu ya kuacha kuwakeketa watoto wadogo, nimeshuhudia hili jambo ni baya, wanatoka damu nyingi sana" amesema Hawa.
0 Comments