Ticker

6/recent/ticker-posts

MHE. BASHUNGWA AFUNGA SHIMIWI KWA KUTOA MAELEKEZO MAHUSUSI YA MIUNDOMBINU YA MICHEZO


****************************

Na. John Mapepele, WUSM

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe Innocent Bashungwa amezitaka Halmashauri zote nchini na Manispaa kuhakikisha viwanja vya michezo, vinakuwa moja ya vipaumbele vya miradi ya maendeleo na kutenga bajeti kila mwaka kujenga, kuboresha, na kulinda viwanja vya michezo.

Mhe. Bashungwa ameyasema haya leo Novemba 2, 2021 wakati alipokuwa akifunga mashindano ya 35 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara (SHIMIWI) mjini Morogoro ambapo amesisitiza kuwa viwanja vikiwa bora ni chanzo cha mapato kwenye Halmashauri, Manispaa na Majiji.

“Mikoa yote ya Tanzania, lazima iboreshe miundombinu ya michezo na mahitaji mengine. Ili watumishi na wananchi waweze kufanya mazoezi na kushiriki kwenye mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi”. Amesisitiza Bashungwa

Aidha, ametoa wito kwa Wenyeviti wa Kamati za Michezo za Mikoa (Ma RAS) na Wilaya (Ma DAS) kuzingatia na kutekeleza maelekezo hayo kwa vitendo kwa kuwa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995, Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa ya mwaka 1967, pamoja na mabadiliko yake anuai, imewapa jukumu ma RAS na ma DAS, kuhakikisha michezo inafanyika na kusimamiwa katika ngazi husika kwa ufanisi.

“Hili litafanikiwa tu ikiwa tutakuwa na miundombinu mizuri. Faida nyingine ni kwamba, tutapunguza majeraha kwa washiriki wa michezo mbalimbali wakiwa uwanjani”amesisitiza Mhe Bashungwa

Akizungumzia kuhusu maelekezo aliyoyatoa Mhe. Dkt Phillip Isidor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati anafungua mashindano haya Oktoba 23, 2021, kuhusu taasisi zote zinazoshiriki mashindano haya kuanza maaandalizi ya michezo hii mapema, Mhe. Bashungwa ameelekeza Watendaji wa Wizara yake kusimamia na kuhakikisha kuwa tabia ya kufanya mazoezi katika maeneo ya kazi inakuwa endelevu.

Pia, kuhusu agizo la Mhe. Makamu wa Rais kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kufanya tathmini ya ushiriki wa kila timu na kuwasilisha taarifa za Wizara, Idara na Taasisi ambazo hazijashiriki. Mhe, Bashungwa amemhakikishi Mhe. Makamu wa Rais, kuwa tathmini hii itafanyika na taarifa itawasilishwa ofisini kwake.

Ameelekeza Wizara, Mikoa na Taasisi zote za Serikali, zijipange kushiriki kwenye michezo ya SHIMIWI ijayo, kwa faida ya wafanyakazi, na ufanisi mahali pa kazi.

Mhe. Bashungwa amemshukuru Mhe. Rais kwa kuridhia kurudisha SHIMIWI ambapo amesisitiza kuwa hatua hiyo ni nzuri, na ishara kuwa washiriki wataongezeka zaidi mwaka ujao, ili kufikia malengo ya Serikali katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kama presha, kisukari na kiribatumbo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela amewashukuru waajiri kwa kuwaruhusu watumishi wao kija kwenye mashindano hjayo ambapo amesema wananchi wa mkoa wake wamenufaika kwa kiasi kikubwa.

Mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa Daniel Mwalusamba amesema uongozi wa SHIMIWI unaiomba Serikali ushiriki wa michezo kwa watumishi wa Serikali kuwa jambo linalotekelezwa kwa mujibu wa sheria.

Mashindano ya SHIMIWI ya mwaka huu 2021 yalishirikisha Wizara 24, mikoa 11, Wakala 4 na Idara 8 za Serikali na yalihudhuriwa pia na Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya TAMISEMI, Viwanda na Biashara na Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mashindano haya yamefufuliwa mwaka huu kufuatia maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu aliyoyatoa Agosti 15, 2021 wakati akishiriki CRDB Marathon akimwakilisha Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Post a Comment

0 Comments