Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wachezaji wa Taifa ya Mpira wa Miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ wakati alipotembelea kuangalia mazoezi na kuwahamasisha kufanya vizuri kuelekea mchezo wa kufuzu kombe la dunia dhidi ya timu ya DR Congo, katika uwanja wa mpira wa Benjamin Mkapa, Novemba Jijini Dar es Salaam 09, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania Kim Paulsen akitoa maelekezo kwa wachezaji wa Taifa ya Mpira wa Miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ katika mazoezi ya time hiyo yanayofanyika katika uwanja wa mpira wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam Novemba 09, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*****************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea mazoezi ya timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Tanzania (Taifa Stars) na amewaeleza wachezaji kwamba Watanzania wanamatarajio makubwa kwamba timu yao itafuzu na kushiriki kombe la Dunia litakalofanyika, Qatar 2022.
“Nimekuja kuona mwenendo wa mazoezi, matarajio tuliyonayo ni makubwa na tuna imani mtashinda. Mechi ya keshokutwa ni muhimu kwa nchi yetu tunahitaji kushinda mechi zilizobaki ili tutimize malengo yetu. Tunahitaji kuweka historia.”
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Novemba 9, 2021) wakati akizungumza na wachezaji wa Timu ya Soka ya Tanzania, (Taifa Stars) katika uwanja wa Benjamin William Mkapa jijini Dar es Salaam baada ya kushuhudia mazoezi ya timu hiyo.
Taifa Stars inafanya mazoezi ya kuajiandaa na michezo ya awali ya kufuzu kombe la Dunia dhidi ya Timu ya Taifa ya DR Congo na Madagascar, ambapo Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza wachezaji wazingatie mafunzo yanayotolewa na walimu.
Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Wizara ya Michezo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wataendelea kuisimamia na kufuatilia maendeleo ya timu hiyo hadi hatua ya mwisho na kuhakikisha inafanya vizuri.
Kwa upande wake, Nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta ambaye amezungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake amesema wamejiandaa vizuri na kwamba watahakikisha wanapata ushindi katika mechi zote zilizobaki. “Tutapambana kwa ajili ya nchi yetu.”
0 Comments