Ticker

6/recent/ticker-posts

MAANDALIZI YA MKUTANO WA MAWAZIRI WA EAC YAKAMILIKA

Na Mwandihi Maalum, Arusha

Mawaziri wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) watakutana jijini Arusha katika Mkutano wao wa 41 wa Baraza la Mawairi uliopangwa kufanyika tarehe 29 Novemba 2021.

Makatibu Wakuu wamekamilisha maandalizi yote yanayohitajika ya mkutano huo, zikiwemo nyaraka za taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Jumuiya, vyombo na Taasisi zake katika kikao kilichofayika tarehe 25 na 26 Novemba 2021.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine ameongoza Makatibu Wakuu wenzake katika kikao hicho, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome; Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro; Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Ikulu, Zanzibar, Bw Mussa Haji Ali na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah.

Mkutano wa Mawaziri ambao utakuwa chini ya uenyekiti wa Kenya unatarajiwa kufanya maamuzi na kutoa maelekezo kuhusu utekeleaji wa masuala ya mtangamano katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya biashara, miundombinu, afya, ajira, fedha na uanzishwaji wa taasisi mpya hususan taasisi za fedha zitakazosimamia Umoja wa Fedha.

Waheshimiwa Mawaziri pia watapitia na kupitisha ratiba ya shughuli za EAC kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2022. Shughuli hizo zinajumuisha mikutano ambapo kwa kanuni za EAC asilimia 50 ya mikutano inafanyika katika nchi wanachama na asilimia 50 iliyosalia inafanyika makao makuu ya Jumuiya. Licha ya makao makuu ya EAC kuwa Tanzania, bado nchi hiyo inapewa mgawo wa mikutano ya asilimia 50 inayofanyika katika nchi wanachama.

Mkutano wa Mawaziri unatarajiwa kuhitimishwa kwa Mawaziri kushuhudia uwekaji saini wa mikataba ya utekelezaji wa majukumu (performance contracts) kati ya Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na Katibu Mkuu wa EAC na baina ya Katibu Mkuu wa EAC na Naibu Makatibu Wakuu na Wakurugenzi wa Idara mbalimbali za EAC.


Meza Kuu wakati wa Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Makatibu Wakuu ikiendesha kikao jijini Arusha.


Ujumbe wa Makatibu Wakuu wa Tanzania ukiwa katika Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Makatibu Wakuu. Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Ikulu, Zanzibar, Bw Mussa Haji Ali na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah.
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Kenya ukifuatilia kikao
Ujumbe wa Tanzania kutoka Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali unaoshiriki mkutano huo.
Wakurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mjadala wa mkutano wa Makatibu Wakuu.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Ellen Maduhu akifuatilia kwa makini mjadala wa mkutano.

Post a Comment

0 Comments