Mhandishi Naomi Mcharo kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, akionesha maeneo ya hifadhi yanayozunguka bwawa la Dongobeshi hayapo katika picha.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Babati Mji Bw. Faustine Masunga, akizungumza kuhusu faida zitokanazo na kilimo cha Umwagiliaji alipokuwa akiongea na waandishi wa Habari ofisini kwake mwishoni mwa wiki.
Picha Ikionesha Bwawa la Dongobeshi linalotumika katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji likiwa katika hali ya upungufu wa maji.
*****************************
Na; Mwandishi wetu – Manyara.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Bi Calorina Mtapula, ametoa wito kwa wakulima wa kilimo cha umwagiliaji Mkoani humo, kutoa tozo na ada zilizopo kisheria katika kilimo cha umwagiliaji, ili kuweza kuchangia maendeleo ya sekta hiyo nchini.
Ameyasema hayo Mkoani Manyara Mwishoni mwa wiki, alipokuwa akizungumza na timu ya watumishi kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na waandishi wa Habari iliyopo Mkoani humo katika kampeni maaalum ya kutoa elimu kwa watendaji na wakulima kuhusiana na swala zima za utoaji wa ada na tozo za umwagiliaji kwa maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji nchini.
Katibu Tawala huyo, amewataka wakulima kulibeba jambo hili na kulifanyia kazi na kusema kuwa ni kwa manufaa yao wenyewe.
“Wakulima tujiunge kwenye vikundi ili tuwezi kuwepo katika skimu na kuweza kupata mavuno na kutoa ada na tozo ambazo zinarudi kwa wakulima wenyewe.” Alisema
Sambamba na hilo Bi Calorie Mtapula, ametoa wito kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Manyara kusimamia kwa kila hali zoezi hilo na kuhakikisha wakulima wanatoa ada na tozo hizo na kuwekwa kwenye mfuko wa maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji. “Isije kutokea 75% ya ada na tozo inayobakia kwa wakulima ikanufaisha watu wachache kwa maslahi yao Binafsi.” Alisisitiza.
Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Babati Mji Bw. Faustine Masunga amesema kuwa, wana jukumu la kuelimisha wananchi na waelewe majukumu yao kama wananchi kwenye swala zima la kilimo cha Umwagiliaji kwani linalenga kupunguza njaa na kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja pato la Halmashauri na Taifa kwa ujumla.
Akiongea wakati timu hiyo ilipotembelea bwawa la Dongobesh, Mhandisi Naomi Mcharo kutoka Tume ya taifa ya Umwagiliaji alisema kuwa Kilimo cha Umwagiliaji ni njia pekee ya kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi , kwani kwa sasa nchi imeingia katika kipindi kirefu cha ukame kilichopelekea upungufu wa maji na mvua.
Amewaasa wanachi wanaozunguka bwawa hilo linalotumika katika shughuli za kilimo, kuachana na shughuli nyingine za kibinadamu katika chanzo hicho na kutunza na kuhifadhi mazingira.
Mhandisi Naomi Mcharo, alisema Tume ya Taifa ya uwagiliaji imejipanga kikamilifu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kumuwezesha mkulima kutumia maji kwa uangalifu, kutumia maji kidogo na kuzalisha zaidi bila kututegemea mvua ambayo kwa sasa imekuwa ni changamoto.Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kutoa elimu ya tozo na ada za umwagilia kwa watendaji na wakulima kwa wilaya zote za mkoa wa Manyara
0 Comments