Ticker

6/recent/ticker-posts

JAJI MAHAKAMA KUU MOROGORO ATANGAZA NEEMA

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe akimsikiliza mmoja wa Waandishi wa Habari aliyekuwa akiuliza swali wakati wa Mkutano na Waandishi hao (hawapo katika picha) uliofanyika tarehe 09 Novemba, 2021 katika Kituo cha Utoaji Haki cha Kanda hiyo.

*******************************

Na Evelina Odemba - Morogoro

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe ameamua kuvalia njuga changamoto ya mlundikano katika magereza yaliyopo mkoani humo ambapo ameahidi hadi kufikia mwezi Machi mwakani tatizo hilo litakuwa na sura tofauti kabisa.

Mhe. Ngwembe ametangaza neema hiyo kwa wafungwa na mahabusu waliopo katika magereza mbalimbali Mkoani Morogoro leo tarehe 9 Novemba, 2021 alipokutana na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali ofisini kwake katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani humo.

“Naomba mnihukumu kuanzia mwezi Machi 2022, ila naahidi kuwa hali haitakuwa kama ilivyo sasa katika magereza yote mkoani humu na hili naomba niwahakikishie kuwa litafanikiwa kwa vile tayari nina takwimu za mahabusu na wafungwa waliopo gerezani,” alisema alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa waandishi hao.

Miongoni mwa maswali hayo ni lililoulizwa na Mwandishi wa Habari kutoka MUM FM, Bw. Rashid Mtagaluka aliyetaka kujua Mahakama katika Kanda hiyo imejipanga vipi kuondoa mrundikano wa mahabusu katika magereza zilizopo mkoani humo.

Mhe. Ngwembe aliongeza kuwa wameandaa mikakati madhubuti kukabiliana na changamoto hiyo, ikiwemo kuwa na kikao cha kimkakati ambacho kitafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 12 Novemba, 2021, na kwamba atakaa na Waheshimiwa Majaji na Mahakimu wote mkoani Morogoro ili kupeana utaratibu wa namna watakavyoenda.

“Siku ya Ijumaa na Jumamosi, Mahakimu wote kuanzia Mahakama ya Hakimu Mkazi mpaka Mahakama za Mwanzo na sisi Majaji wa Mahakama Kuu tutakuwa na kikao kujadili kwa kina jambo hili, hivyo mtu asifike Mahakamani siku hiyo akitegemea atamkuta Hakimu. Tunataka tuondokane kabisa na changamoto hii,” amesema.

Jaji Mfawidhi huyo alitumia nafasi hiyo kuomba ushirikiano kutoka kwa Waandishi wa Habari hao ili kuhabarisha shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama na kufikisha elimu ya sheria kwa wananchi.

Mhe. Ngwembe alielezea nia yake ya kukutana nao ambayo, pamoja na mambo mengine, ni kuweka mikakati ya namna watakavyoshirikiana ili kuwafikishia wananchi habari mbalimbali zinazohusu Mahakama ya Tanzania.

Alifafanua kuwa miongoni mwa matukio mengi yanayotokea katika jamii yanachangiwa na aidha wananchi kutokuwa na elimu sahihi au kutoijua sheria vizuri, huku akitolea mfano wimbi la watoto wa mitaani na matukio yanayochangiwa na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.

“Tunawaombeni sana muweze kushirikiana na Mahakama ili tuweze kutoa elimu hii kupitia vyombo vyenu vya habari. Hatua hii itasaidia sana wananchi kuelewa hatua za kisheria ambazo wanaweza kuchukua na hivyo kupunguza migogoro mbalimbali katika jamii,” Jaji Mfawidhi huyo alisema.

Mhe Ngwembe anatarajia kuanza ratiba maalumu ya kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari vilivyopo mkoani Morogoro na ratiba hiyo inatarajiwa kuanza hivi karibuni ikiwa imelenga maswala mbalimbali yakiwemo ulinzi wa watoto, vifo na mirathi, ndoa na talaka, haki ya kusikilizwa na kuwasilisha mada mbalimbali za kisheria zitakazoisaidia jamii.

Post a Comment

0 Comments