Afisa mazingira kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Jeremiah Legela akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi (hawapo pichani) yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya mji wa Geita Mkoani Geita Novemba 15, 2021.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya mji wa Geita Mkoani Geita Novemba 15, 2021.
Kaimu Mkuu wa kitengo cha mazingira Wizara ya Mifugo na Uvuvi, (Mifugo) Bw. Yusuf Selenge (wa nne kutoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya geita mara baada ya mafunzo mafupi ya kuongeza uelewa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa watendaji hao yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya mji wa Geita Mkoani Geita Novemba 15, 2021.
**********************************
Halmashauri zote nchini zimehimizwa kuzingatia mipango bora wa matumizi ya ardhi ikiwemo kuweka njia za Mifugo zitazowawezesha kwenda kwenye Malisho, maji na kwenye Masoko Ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Rai hiyo ilitolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha mazingira Wizara ya Mifugo na uvuvi Sekta ya Mifugo, Bw. Yusuf Selenge katika mafunzo ya ufugaji endelevu unaokabili mabadiliko ya tabia nchi yaliyofanyika Mkoani Geita Novemba 15, 2021.
Akiongea katika mafunzo hayo alisema kuwa asilimia kubwa ya migogoro inatokana na baadhi ya vijiji kutokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi na kusabisha njia za kupitisha mifugo ikitumika kwa matumizi mengine.
“hii programu itasaidia sana kwa sababu imehimiza matumizi bora ya ardhi kwa hiyo Halmashauri wanatakiwa kutafuta wafadhiri na mapato yao ya ndani kuweza kutekeleza mpango huo kwa sababu njia za kupitisha mifugo zilikuwepo lakini zimevamiwa kwa matumizi mengine," alisema
Kuhusu mradi wa utekelezaji wa mradi wa ufugaji endelevu, Selenge alibainisha kuwa programu hiyo inatekelezwa katika sekta tatu za kilimo, mifugo na uvuvi ambapo kwa sasa mafunzo hayo yanatolewa kwa maafisa katika Halmashauri ambao watawajibika kufikisha elimu kwa wakulima na wafugaji ngazi za vijiji.
Aliongeza kwa kusema kuwa programu hiyo ilianza kutekelezwa tangu 2015 hadi 2025 ambapo utekelezaji wake unafanyika katika mamlaka ya Serikali za mitaa kupitia kwa maafisa sita katika halmashauri ambao watawajibika kufikisha elimu kwa wakulima na wafugaji.
“Halmashauri ndio wanachukua elimu hii na kuifikisha ngazi ya kata na kijiji, maafisa tunaofanya nao ni sita kwenye Halmashauri ambao ni Afisa Mazingira, Afisa mifugo na uvuvi, Afisa kilimo na umwagiliaji, Afisa malisho, Afisa mipango pamoja na Afisa maendeleo ya jamii,” aliongeza
Aidha Bw. Selenge aliwahimiza maafisa hao wa Halmashauri kuhakikisha wanawaelimisha wafugaji njia bora ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo kuwashauri wananchi kuhimilisha Mifugo yao, kulima Malisho, kuyaboresha, kuyahifadhi, na kuvuna maji.
Naye, Afisa Mazingira kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Jeremiah Legela alisema kuwa pamoja na mambo mengine mafunzo hayo yatasaidia kuboresha mifugo ikiwemo kutoweka chapa katika mifugo ambayo imekuwa ikiharibu ngozi na kupunguza ubora.
Aliongeza kuwa mpango wa sasa ni kutumia njia ya kisasa ikiwemo kuweka hereni katika masikio na kuiacha ngozi ya mifugo zikiwa na ubora ambapo unahitajika katika soko hasa viwanda vya ngozi vilivyopo nchini.
Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Bi. Mpelwa James alibainisha kuwa faida waliyoipata katika mafunzo hayo watahakikisha inawafikia wafugaji ili kuhakikisha wanashiriki kulinda mazingira hasa katika vyanzo vya maji.
“kitu ambacho nimeondoka nacho hapa cha kwenda kufanya kwa wafugaji ambao wana mifugo mingi zaidi ya elfu moja ni kuwahimiza na kuwashirikisha kufanya tathimini za kimazingira ili kukabiliana na ya athari za mabadiriko ya tabia ya nchi kwa sababu wasipofanya hivyo kutakuwa na hatari ya kukosa malisho,” alisema
Aliongeza kuwa hatua hiyo itawaongezea uelewa wananchi juu ya mabadiriko ya tabia ya nchi na itawajengea uwezo wa kuhimili mabadiliko hayo ili waweze kuwa na uhakika wa kupata chakula cha mifugo na kwenye kaya zao kutokana na uzalishaji wenye tija.
0 Comments