******************
Na. Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), leo Novemba 19, 2021 imekabidhi vifaa vya kutolea huduma ikiwemo dawa ya Methadoni kwa waathirika wa dawa za kulevya katika Gereza la Segerea na Sehamu zingine ambazo zinatumika kamam vituo vidogo vya kutolea huduma za Methadoni kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza katika Hafla hiyo iliyofanyika katika Gereza la Segerea Jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Gerard Kusaya amesema kuwa tukio hilo ni muhimu na serikali kupitia mamlaka itaendelea kuwasaidia na kuwaelisha waraibu wa dawa za kulevya ili kuokoa nguvu kazi ya taifa.
“Tuna tukio moja la aina yake hapa Segerea Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, leo inakabidhi vifaa hivi ambavyo vitatumika kutoa huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya walioko humu lakini pia na wengine ambao wameathirika pia watatumia kituo hiki kidogo cha kutoa huduma hiyo (Satellite Clinic) ili warudi katika hali zao za kawaida” Alisema Kamishna Jenerali, Kusaya.
Kusaya alisema kuwa mpaka sasa Tanzania kuna vituo vikubwa vya kutolea huduma hiyo vipo 11 huku akiwaomba watanzania kuacha mara moja tabia ya kuuza na kusambaza dawa za kulevya kwani kufanya hivyo ni kuharibu nguvu kazi ya vijana.
Aidha, Kusaya alisema kuwa mpaka sasa vituo vya matibabu ya Methadoni vinahudumia watu 10,600 ambao wameathirika na dawa za kulevya kwa hiyo idadi hiyo ni kubwa ukilinganisha na vituo vinavyotoa huduma hiyo.
Alivitaja vituo vidogo vya kutolea huduma ya Methadoni (Satellite Clinic), kwa Dar es Salaam kwani ndiyo mkoa unaoongoza kwa uraibu wa dawa za kulevya ni pamoja na Segerea-Ilala, Vijibweni-Kigamboni, Temeke na Tegeta- Kinondoni.
Aliongeza kuwa zoezi la ugawaji vifaa na kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya na kuwarudisha katika hali yao ya kawaida ni zoezi endelevu na Mamlaka itahakikisha kuwa inaanzisha vituo vikubwa katika kila mkoa nchini.
“ Zoezi hili ni endelevu hapa tumetoa vifaa na dawa ya Metahdoni, vifaa tulivyotoa ni pamoja na Kasiki moja ya kuhifadhia dawa, vitanda, mashine ya kuotolea kopi, mashine ya kuchapisha, dawa ya methadone, viti vya kawaida na viti vya kiofisi, kwa hiyo vitu hivi vitatumika kutoa huduma hapa Gereza la Segerea”, Alisema Kamishna Jenerali, Kusaya.
Kamishna Jenerali alitoa rai kwa watanzania waache kufanya biashara na kutumia dawa za kulevya kwani Mamlaka ipo macho na itawachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kufungwa jela, lakini pia biashara hiyo inaharibu nguvu kazi ya taifa.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Magereza Dar es Salaam, ACP. Focus Ntakandi alisema kuwa jambo la kutoa vifaa kwa magereza ili kuwasaidia wafungwa ambao wameathirika na dawa za kulevya ili kuwarahisishia kufanya kazi zao.
“Ujio wako kwetu ni jambo kubwa sana kwa sababu tumekaa na watu ambao wanamatatizo ya dawa za kulevya na wanakuwa wamebadilika akili na kuwa kama mazezeta kwa hiyo huduma hii itakuwa msaada kwao na kutusaidia sisi kufanya kazi zetu vizuri”, Alisema ACP. Ntakandi.
Aliongeza kuwa Mamlaka inatakiwa iongoze huduma hiyo kwa kuweka vituo vingine katika magereza mbalimbali lengo likiwa ni kuwasaidia kusafirisha watu hao kutoka sehemu nyingine kwenda sehemu nyingine bila usumbufu.
0 Comments