Ticker

6/recent/ticker-posts

CHANDE AZINDUA MRADI WA “UREJESHWAJI ENDELEVU WA MAZINGIRA NA HIFADHI YA BIOANUAI” JIJINI MBEYA.


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande akizungumza wakati wa warsha ya kuzindua mradi wa ‘Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai’ iliyofanyika jijini Mbeya leo Novemba 11, 2021.


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande akizungumza wakati wa warsha ya kuzindua mradi wa ‘Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai’ iliyofanyika jijini Mbeya leo Novemba 11, 2021.


Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga akimkaribisha Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande kuzungumza wakati wa warsha ya uzinduzi wa mradi wa “Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai’ iliyofanyika jijini Mbeya leo Novemba 11, 2021.


Mgeni rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande (waliokaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali na washiriki wa warsha uzinduzi wa mradi wa ‘Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai’ iliyofanyika jijini Mbeya leo Novemba 11, 2021.

******************************

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande amesema uharibifu wa misitu nchini imekuwa ni kubwa na hivyo kutishia usalama wetu.

Chande amesema hayo leo Novemba 11, 2021 alipokuwa akizungumza wakati akizindua Mradi wa “Urejeshwaji endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai” iliyofanyika jijini Mbeya.

Alisema tafiti zimebainisha kuwa kila mwaka nchi yetu hupoteza wastani wa takriban hekta 469,420 za misitu na upotevu huo umesababisha upotevu mkubwa wa bioanuai na hatari ya kutoweka kwa baadhi ya aina muhimu za jamii ya mimea na wanyama.

“Kama kasi ya uharibifu wa mazingira isipodhibitiwa, nchi yetu itakuwa katika hatari ya kugeuka jangwa kwa mfano tathmini iliyofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii imeonesha hali ya uharibifu ikiendelea hivyo, katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2033, uharibifu wa misitu utaigharimu Serikali kiasi cha shilingi bilioni 167 za kurejesha mazingira katika hali yake. Kiasi hiki kingeweza kufanya shughuli za kimaendeleo katika taifa letu kama tutatunza mazingira vizuri,” alisema Chande.



Naibu Waziri Chande aliongeza kuwa nchi yetu inakadiriwa kuwa na hekta millioni 48.1 za misitu sawa na wastani wa asilimia 51 ya eneo lote la nchi kavu ambayo ina manufaa makubwa katika hifadhi ya bionuai ikiwemo makazi ya viumbe hai, vyanzo vya maji, husaidia kupunguza joto ukaa na zaidi ni husaidia kutunza ardhi yetu kuwa na rutuba.



Aidha, aliwakumbusha kuwa Serikali haitavumilia kuona ubadhilifu wa aina yoyote katika utekelezajiwa mradi huu na kwua Ofisi ya Makamu wa Rais itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha thamani ya fedha inaendana na miradi itakayotekelezwa katika maeneo yetu.

Awali akitoa neno la ukaribisho, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga alibainisha kuwa Mradi huo unaofadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 11.2 sawa na sh. Bilioni 25.7.

Alisema lengo la mradi huu ni kuimarisha usimamizi wa pamoja wa mazingira na urejeshwaji wa ardhi iliyoharibika ili kuleta ustawi wa mifumo-ikolojia na jamii kwa ujumla na ni sehemu ya mradi mkubwa wa kidunia (The Global Groject) unaotekelezwa katika nchi 11 duniani ikiwemo Tanzania.

Bi. Maganga alishukuru GEF na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa kushirikiana na Serikali kupata fedha za utekelezaji wa mradi huu pamoja na Shirika la IUCN kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais katika hatua zote za maandalizi ya mradi.

Post a Comment

0 Comments