Ticker

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAANIKA ITAKAVYOTUMIA TZS BIL.90.2


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaaam leo Oktoba 17, 2021jinsi itakavyotumia Shilingi bilioni 90.2 za mgao wa mkopo wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) katika maeneo makuu matano ambayo yameathirika zaidi kutokana na ugonjwa wa UVIKO-19

**************************

Wizara ya Maliasili na Utalii imesema itazitumia Shilingi bilioni 90.2 za mgao wa mkopo wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) katika maeneo makuu matano ambayo yameathirika zaidi kutokana na ugonjwa wa UVIKO-19 ikiwemo kukarabati na kujenga miundombinu ya utalii katika maeneo ya hifadhi za Taifa ili kuongeza watalii wanaoitembelea Tanzania.

Hatua hiyo imekuja kufuatia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata mkopo wenye masharti nafuu wa shilingi Trilioni 1.3. kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 ambao umeelekezwa kwenye baadhi ya Wizara zikiwemo TAMISEMI, Afya, Elimu na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaaam leo Oktoba 17, 2021. Amesema eneo la kwanza litakuwa ni Kuziwezesha Taasisi za Wizara zilizoathirika zaidi kutokana mlipuko wa UVIKO-19 ambazo ni TANAPA, TAWA, NCAA, TFS na Makumbusho ya Taifa ziweze kutekeleza majukumu ipasavyo kwa kuziwezesha kuboresha miundombinu na kununua vifaa mbalimbali.


“Kupitia fedha hizi tutajenga na kukarabati barabara zenye urefu wa kilometa 4,881, barabara hizi zitachochea shughuli za utalii ambazo zimetetereka na kuwezesha watalii kuingia katika hifadhi zetu, janga la Uviko-19 lilisabaisha kupungua kwa watalii na mapato yatokanayo na utalii kiasi cha kuzifanya taasisi za uhifadhi zishindwe kujiendesha na miundombinu kuharibika,” amesema Dk Ndumbaro.

Amesema uboreshaji huo wa miundombinu utafanyika katika hifadhi za Taifa za Serengeti, Mkomazi, Katavi,Tarangire, Nyerere, Kilimanjaro, Saadani, Gombe, Ngorongoro pamoja na maeneo ya Misitu Asilia 10 inayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu -TFS.

Dkt. Ndumbaro ameeleza kuwa fedha hizo zitatumika katika ununuzi wa mifumo ya kielektroniki kufanya ufuatiliaji katika taasisi mbalimbali, mitambo ya ujenzi, kukarabati na kujenga viwanja vya ndege nane ndani ya hifadhi za Taifa ikiwemo Serengeti na kujenga malango matano katika baadhi ya hifadhi.

Sambamba na hilo wizara hiyo inaenda kuboresha na kudhibiti ubora wa huduma za utalii ambazo zimeshuka wakati wa Uviko-19 ikiwemo hoteli, kutoa mafunzo na kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato katika vituo vya utalii.

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, idadi ya watalii imeongezeka mwaka huu na inaweza kuvuka matarajio ya awali yaliyowekwa. Kati ya Januari hadi Septemba 30 mwaka huu, Tanzania imepokea watalii wa kimataifa 623,800.


Idadi hiyo iko juu ikilinganishwa na watalii 620,000 walioingia Tanzania kati ya Januari na Desemba mwaka jana. Dkt. Ndumbaro amesema Wizara itaimarisha masoko na kutangaza utalii ambapo kwa kukarabati vituo saba vya urithi wa kiutamaduni na kununua vifaa kwa ajili ya kutolea taarifa za utalii kwa njia ya kidijitali


Tunafahamu “Royal Tour” ameianzisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akaifikisha mahali, sisi hatutaki ipoe, tunakwenda kutanua wigo wa “Royal Tour” kutangaza zaidi vivutio na maeneo mbalimbali” amesema Dk Ndumbaro.
Pia Wizara itashiriki na kuwezesha maonesho makubwa mawili ya utalii ya kimataifa ili kutangaza zaidi vivutio vya utalii.

“Eneo tatu tunakwenda kuimarisha mazingira ya biashara ya utalii kwa kuhakikisha kwamba usalama na huduma za afya katika vituo vya utalii zinakuwa katika kiwango cha kimataifa,” amesema waziri huyo.

Amesema hakuna mtalii atakayekuja Tanzania kama usalama na huduma za afya zinalega lega.“Kwenye hili tutashirikiana na wenzetu wa Tamisemi kwa kufuata miongozo iliyotolewa na Wizara ya Afya. Tutaendelea kusisitiza upatikanaji wa chanjo katika maeneo ya utalii,” amesema Dk Ndumbaro na kuongeza kuwa fedha hizo zitawezesha kuwepo kwa vifaa vya kupima Uviko-19 katika vituo vya utalii.

Post a Comment

0 Comments