Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI CHANDE AZITAKA HALMASHAURI KUZIBANA KUMBI ZA STAREHE ZINAZOPIGA KELELE MAENEO YA MAKAZI

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande akizungumza katika moja ya mikutano ya Kamati ya Mawaziri 8 wa Wizara za Kisekta kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi mwishoni mwa wiki.
Sehemu ya wananchi wakimskiliza Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande wakati wa ziara ya Mawaziri 8 wa wizara za kisekta kuhusu mgogoro wa matumizi ya ardhi mkoani Mara mwishoni mwa wiki.


*******************************


Na Munir Shemweta, WANMM GEITA

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande amezitaka halmashauri nchini kuhakikisha zinadhibiti nyumba za starehe zinazopiga muziki wa kelele katika maeneo ya makazi ya watu.

Alisema, kuna baadhi ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya makazi lakini ghafla maeneo hayo yanatumiwa kwa shughuli zisizopangwa kama vile kumbi za starehe na kuleta usumbufu wa kelele kwa wananchi.

"Katika halmashauri kuna maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya makazi na shughuli nyingine lakini ghafla maeneo hayo yanabadilika na kuwa kumbi za starehe zinazopiga muziki unaoleta kelele na kukera watu, huu muhali tuuondoe" alisema Chande.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, halmashauri nchini zinatakiwa kusimamia mipango yake kwa kuhakikisha shughuli zinazofanyika katika maeneo yake ni zile zilizopangwa kwa kuwa mara kadhaa kumekuwa na malalamiko kuhusu muingiliano wa nyumba za makazi na kumbi za starehe.

Waziri Chande ambaye alikuwa akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa kikao kati ya Kamati ya Mawaziri 8 wa Wizara za Kisekta na viongozi wa mkoa wa Geita alisema, nyumba za starehe zinazopiga kelele za muziki kwenye maeneo ya makazi zimekuwa zikileta athari ikiwemo kwa wagonjwa wa moyo na kuzua malalamiko miongoni mwa wananchi ambapo alizitaka halmashauri zote nchini kutofumbua macho suala hilo.

Alisisitiza kwa kusema kuwa, kama nyumba imepangiwa matumizi ya makazi basi itumike kwa suala hilo na si vinginevyo na kubainisha kuwa, halmashauri zihakikishe zinaandaa na kusimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo yake.

Akigeukia suala la usimamizi wa mazingira nchini Chande alisema, mazingira ndiyo maisha na uhai wa binadamu na viumbe vingine hivyo wananchi wanatakiwa kuhakikisha wanayatunza ili kuepuka kukosa rasilimali hewa.

" Ukikosa rasilimali hewa uhai na thamani ya ubinadamu imeisha na bila mazingira hakuna mifugo wala maji, mazingira yetu ndiyo maisha na uhai wetu" alisema Chande.

Awali mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri 8 wa Wizara za Kisekta katika utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema, katika mkoa wa Geita imeamuliwa vijiji 37 vilivyokuwa kwenye mgogoro wa muda mrefu na maeneo ya hifadhi za misitu vibaki katika maeneo yake.

Aidha, serikali imeamua kumega sehemu ya hifadhi za misitu 9 katika mkoa wa Geita kwa ajili ya kuwapatia wananchi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hizo.

Ametaja hifadhi za misitu zilizomegwa kuwa ni Geita, Ruande, Rwamgasa, Usindakwe na Miyenze zilizoko wilayani Geita, hifadhi ya Mbogwe iliyopo halmashauri ya wilaya ya Bukombe, Biharamulo-Chato pamoja na hifadhi ya misitu ya Runzewe na Ushirombo zilizopo wilaya ya Bukombe.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, tathmini ya kina itafanyika katika hifadhi hizo ili kujua kiasi cha hifadhi ya msitu itakayomegwa na matumizi yake kama vile kilimo, ufugaji na makazi.

" Tume ya kufanya tathmini tutakayoiacha hapa itarejea mipaka ya vijiji vinavyopakana na hifadhi na kumega maeneo ya hifadhi na kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijjji vinavyopakana na hifadhi hizo" alisema Waziri Lukuvi.

Alisema, timu hiyo ya kufanya tathmini itafanya marejeo ya matangazo ya serikali ya misitu iliyomengwa na kuweka alama za kudumu za mipaka.

Post a Comment

0 Comments