Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbertm Makoye akieleza mafanikio ambayo Tamasha la Bagamoyo limeyapata kwa kipindi cha miaka 40 wakati alipoongea na vyombo vya habari katika Chuo cha Sanaa Bagamoyo.
******************************
Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo.
TAMASHA kubwa la kila mwaka la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo linatarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia 28 hadi 30 Oktoba mwaka huu katika viwanja pamoja na ufukwe wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) liwa na kauli mbiu ya 'Sanaa ni ajira'.
Katika kunogesha na kufikia malengo ya tamasha hilo ambalo kwa msimu huu ni la 40, Wasanii na wadau mbalimbali wa sanaa nchini na nje ya nchi wamehimizwa kujitokeza kushiriki ilikujionea urithi wa sanaa za Utamaduni hapa nchini.
Akizungumza na Wanahabari mapema leo, katika ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Bi. Zainabu Abdallah alisema Serikali na Taasisi zake wanaunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, kwa vitendo kwa kuendelea kutangaza fursa zilizopo katika mji wa Bagamoyo kupitia Tamasha hilo ambalo ni fursa kwa wasanii na wafanyabiashara pia.
Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa, katika tamasha hilo wanatarajia ushiriki wa viongozi mbalimbali wa kitaifa, mabalozi, wakuu wa mikoa, wakuu wa Wilaya, wabunge pamoja na viongozi mbalimbali kutoka Taasisi za Serikali na Sekta binafsi.
Mhe. Zainabu alibainisha kuwa, kuwa tamasha litarushwa mubashara na baadhi ya vyombo vya habari nchini ili kuwapa fursa wanachi ambao hawataweza kufika waweze kuona tamasha wakiwa majumbani au sehemu nyingine.
“Hivyo tamasha hili litaonekana dunia nzima na hii inaitoa Bagamoyo na kuiweka kwenye ramani, dunia na Tanzania waweze kujua fursa zilizoko Bagamoyo,” akisema Mhe. Zainabu.
Mkuu wa Wilaya alimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo Dkt. Hassan Abasi kwa kushirikiana na TaSUBa pamoja na Serikali ya Wilaya Bagamoyo kuhakikisha Tamasha la Sanaa Bagamoyo linafanyika.
Awali akimkaribisha mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbert Makoye alisema Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo mwaka huu litafanyika kuanzia tarehe 28.10.2021 hadi 30.10.2021 katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).
Dkt. alisema Tamasha hili linabeba kaulimbiu isemayo, “Sanaa ni Ajira” ikiwa ni mahsusi katika kuonyesha kuwa sanaa ni zaidi ya burudani, inaweza kuwa ajira au biashara na chanzo cha kipato kwa msanii.
Dkt. Makoye alisema Tamasha hili hufanyika kila mwaka na huandaliwa na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) chini ya Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo.
Dkt. Makoye alifafanua kuwa dhumuni la Tamasha ni kutunza na kuenzi sanaa na utamaduni wa mtanzania, kutengeneza jukwaa ambalo wanafunzi wa TaSUBa wanalitumia kupima viwango vyao vya umahiri katika sanaa kwa mwaka katika fani za sanaa za maonyesho na zile za ufundi.
Aliongeza kuwa lengo linguine la Tamasha ni kukutanisha watu wa tamaduni mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali za dunia ili kuonyesha utajiri wao wa sanaa na utamaduni, kutengeneza jukwaa ambalo ni kiungo cha kujenga mahusiano ya wasanii wa ndani na nje ya nchi kupitia maonyesho ya sanaa, pia kubadilishana uzoefu na mawazo katika kuendeleza tasnia ya sanaa na kutoa burudani kwa watanzania na wageni.
“Tamasha la mwaka huu litapambwa na ngoma za asili, muziki wa kizazi kipya, singeli, sarakasi, mazingaombwe, maigizo pamoja na maonyesho na biashara ya sanaa za ufundi". Alisema Dkt. Makoye.
Aidha alibainisha kuwa, jumla ya vikundi ambavyo vimethibitisha kushiriki mpaka sasa ni 70, ambapo vikundi vya ndani ya nchi ni 60 na vikundi 10 kutoka nje ya nchi (India, Malawi na Mayotte).
Pamoja na burudani hizo, kutakuwa pia na vyakula vya asili pamoja na vinywaji vya asili.
Naye Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Kiagho Kilonzo amesema Taasisi hio inaungana na TaSUBa katika kufanikisha Tamasha la 40 la Sanaa na Utamaduni ambapo katika kutekeleza hilo kutakua na hema kwa ajili ya kuonyesha filamu ambalo litabeba watu takribani mia moja.
Ndani kutakua na screen kubwa ambazo zitaonyesha filamu. Lengo kubwa likiwa ni kuendeleza na kudumisha filamu.
"Kutakua na wasanii wa filamu kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania hususani jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuipendezesha siku hiyo na kuleta hamasa kwa vijana." alisema Dkt. Kilonzo.
Aidha Kaimu Katibu Mtendaji, Baraza la Sanaa Tanzania Bw. Matiko Mniko alisema tamasha la Bagamoyo ni fursa nzuri kwa Tanzania kuinua utalii wa utamaduni nchini.
0 Comments