Ticker

6/recent/ticker-posts

TAKRIBANI WANANCHI 11,636 WAPATIWA ELIMU YA VIWANGO


Afisa Udhibiti Ubora (TBS), Bw. Stanford Matee akitoa elimu kwa wananchi jinsi ya kutambua bidhaa zilizothibitishwa ubora na umuhimu wa kusoma taarifa za mzalishaji na muda wa mwisho wa matumizi katika Gulio la Mamsera wilayani Rombo wakati wa kampeni ya elimu kwa umma. Maafisa wa TBS wakitoa elimu ya namna ya kutambua bidhaa zilizothibitishwa ubora wake na TBS na madhara yanayoweza kutokea kwa kutumia bidhaa zisizo na ubora kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari Katesh wakati wa kampeni ya kuelimisha umma wilayani Hanang.

***************************

Na Mwandishi Wetu

Wananchi 11,636 kati yao 7,536 wakiwa ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika wilaya za Lushoto, Rombo na Hanang wamepati elimu kuhusu umuhimu wa kununua bidhaa zilizothibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) sambamba na kuwahamasisha wafanyabiashara kusajili maduka ya chakula na vipodozi.

Wananchi hao walipatiwa elimu hiyo kupitia kampeni ya kutoa elimu kwa umma iliyoendeshwa na shirika kwenye wilaya hizo ambayo imelizika mwishoni mwa wiki.

Kampeni hiyo ya elimu kwa umma ilifanyika katika maeneo mbalimbali kwenye ya shule za msingi na sekondari, masoko, stendi, minadani na maeneo mengine ya wazi ambapo wananchi walijitokeza kwa wingi kupata elimu na ufahamu wa masuala mbalimbali yahusuyo ubora wa bidhaa.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Masoko wa TBS, Gladness Kaseka aliwakumbusha wananchi kuwa vita ya bidhaa hafifu sio ya TBS pekee, bali ni ya Taifa kwa ujumla.

"Kampeni hii imeweza kuwafikia wananchi 11,636 kati yao wanafunzi wa shule za msingi na sekondari 7,536 na wananchi 4100," Alisema Kaseka.

Kaseka aliwafafanulia wanafunzi pamoja na walimu umuhimu wa viwango katika maisha yao ya kila siku vilevile kuwafahamisha fursa ya huduma bure kwa wajasiriamali wadogo.

Alitaka wawe mabalozi wazuri wa kuhamasisha ubora katika jamii wanazoishi.

Vilevile aliwasisitiza wananchi kuendelea kutoa taarifa pindi wanapokutana na bidhaa zilizokwisha muda wake au wanapotilia shaka bidhaa yoyote katika soko au ziĺizopigwa marufuku kama vile nguo za ndani za mitumba, mafuta ya breki dot 3 na baadhi ya vipodozi.

Alitoa mwito kwa wafanyabiashara kufuatilia taratibu sahihi za usajili wa bidhaa au majengo kupitia mawasiliano waliyopewa pamoja na kutembelea ofisi ya TBS iliyopo karibu au kupiga katika kituo cha huduma kupitia mawasiliano waliyopewa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Lushoto, Ikupa Mwaisyoge aliipongeza TBS kwa kutoa elimu hiyo kwa wananchi katika ngazi ya wilaya, kwani itaongeza ufahamu na kuhakikisha suala la uuzaji wa bidhaa hafifu sokoni linapungua kama sio kwisha kabisa.

"Niwaombe TBS kutoa mafunzo katika vikundi vya wajisiriamali wilayani Lushoto ili waweze kuanza mchakato wa kupata leseni ya kutumia alama ya ubora," alisema Mwaisyoge.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mkalema wilayani Rombo, Gerson Temu aliipongeza TBS kwa kazi nzuri wanaoifanya na kutoa wito iendelee na kasi hiyo hiyo ya utendaji na hasa kaguzi za mara kwa mara wilayani. Kampeni hiyo itaendelea katika Wilaya za Mlele Nkasi na Kasulu.

Post a Comment

0 Comments