Ticker

6/recent/ticker-posts

NMB YAZINDUA HATI YA KIAPO CHA HUDUMA KWA WATEJA



Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe Anthony Mtaka (wa tatu kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kushoto) wakizindua Hati ya Kiapo cha Huduma kwa Mteja wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na benki hiyo kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja iliyofanyika jijini Dodoma leo. Wengine kutoka kulia ni; Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara Benki ya NMB, Filbert Mponzi; Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mhe. Mwanahamisi Mukunda; Mbunge wa Bahi, Mhe. Kenneth Nollo na Mbunge wa Dodoma Mjini, Mhe. Anthony Mavunde.




****************************************

Benki ya NMB imezindua maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja kwa kuahidi kuendelea kuwahudumia wateja wake kwa viwango bora ili kudumu katika nafasi yao kama taasisi ya fedha pendwa na inayoongoza nchini.



Ahadi hiyo ipo kwenye Hati ya Kiapo cha Huduma kwa Mteja ambayo benki hiyo iliizindua sambamba na uzinduzi wa shughuli za wiki ya wateja jijini Dodoma leo.



Katika hafla hiyo na kama sehemu ya sherehe za kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja, NMB pia ilitoa misaada mbalimbali mkoani humo yenye thamani ya TZS 40 milioni yakiwemo madawati na vifaa vya hospitali.



Shughuli kama hizo zilifanyika katika kanda zote za benki hiyo nchini zikiongozwa na viongozi wa ngazi za juu ambako pia misaada mbalimbali ilitolewa.



Mgeni rasmi jijini Dodoma alikuwa Mkuu wa Mkoa, Mhe. Anthony Mtaka. Tukio hilo pia lilihudhuriwa na wabunge wa Mkoa wa Dodoma, wakuu wa wilaya, wateja wa NMB na viongozi mbalimbali walioipongeza benki hiyo kwa ubunifu na ubora wa huduma zake huku wakisema uwekezaji inayoufanya katika maendeleo ya taifa ni mkubwa na wa kuigwa.



Bi. Zaipuna alisema Hati ya Kiapo cha Huduma kwa Mteja ni nyenzo muhimu katika kuweka uhusiano mzuri na wateja wa benki hiyo ili waendelee kuiamini na iweze kuendeleza ushindani wenye tija sokoni. Mkataba huo wa hiari pia unaiwezesha NMB kuweka maazimio ya uhusiano wa kibiashara wenye afya na wateja wake.



“Leo tunaungana na dunia nzima kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja, inayoadhimishwa kila mwaka wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba,” Bi Zaipuna alisema.



“Kauli mbiu ya Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa mwaka huu ni ‘Nguvu ya Huduma’ na ili NMB iendelee kuongoza kwenye utoaji huduma kwa wateja, maadhimisho haya tunayatumia kuzindua Hati ya Kiapo cha Huduma kwa Mteja kuonyesha kwa vitendo nguvu ya huduma kwa wateja wetu,” kiongozi huyo alifafanua.



Bi Zaipuna alisema kimsingi hati hiyo ina ahadi tano za benki kwa mteja ambazo ni kupatikana kwake kwa haraka, usikivu, uhakika na kuaminika, usalama wa taarifa za mteja pamoja na weledi na nidhamu.





Akiwapongeza wateja kwa kuiunga mkono benki hiyo na kuchangia mafanikio yake, Bi Zaipuna alifafanua kuwa ahadi hizo ni maazimio yatakayolinda haki ya mteja na pia yenye kudhamiria kudumisha uhusiano wao mzuri..



“Mbali na wateja, naomba pia niwashukuru wafanyakazi wenzangu wa Benki ya NMB kwa kazi kubwa wanayofanya, benki hii imekuwa ikiongoza kwa kila kitu sababu ya utendaji mzuri na uaminifu wao, na ndiyo nguzo tunayosimamia,” alisisitiza.



Bw Mtaka aliitaka NMB kutochoka na ukarimu wake ambao hata viongozi wengine walisema umekuwa ni chachu kubwa ya kuyabadilisha maisha si tu ya wakazi wa Dodoma bali pia Tanzania nzima.



“Suluhishi zenu bunifu za kifedha na uwekezaji mkubwa mnaoendelea kuufanya ni vitu vinavyoifanya NMB kuwa benki kubwa na kiongozi wa maendeleo nchjini,” Mhe. Mtaka alisema.



Misaada ambayo NMB iliitoa leo Dodoma ni pamoja na vifaa vya hospitali kwa ajili ya Hospitali Wilaya ya Bahi na Zahanati ya Chimedeli. Pia vimo viti 200 na meza 200 kwa ajili ya shule za sekodari Nondwa, Msisi Juu, Sechelela na Ibihwa pamoja na madawati 50 kwa ajili ya Shule ya Msingi Chiguluka na mabati kwa ajili ya Shule ya Sekondari Bahi.

Post a Comment

0 Comments