*********************
Na WAMJW - Kilimanjaro
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi Mhe. Fatuma Toufiq ameitaka Serikali kuharakisha mchakato wa kuifanya Hospitali ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto kuwa Taasisi kamili mapema.
Mhe. Toufiq ametoa kauli hiyo leo wakati wa ziara ya Kamati katika Hospitali ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi ya Kibongóto iliyopo Wilaya ya Siha Mkoa wa Kilimanjaro kuona hali ya utoaji wa huduma za tiba pamoja na ukaguzi wa miradi ya maendeleo.
“Mimi na Kamati hili tunasema kwamba jambo hili la Kibong’oto kuwa Taasisi tumelichukua na tutahakikisha tunaenda kuishauri Serikali kuharakisha mchakato wa kuifanya Hospitali hii kuwa taasisi kamili” amesema Mhe. Toufiq mara baada ya kupokea ombi la Hospitali hiyo kuwa Taasisi kamili kutoka kwa uongozi wa Hospitali hiyo.
Hata hivyo Mhe. Toufiq hakusita kuwapongeza watumishi katika Hospitali hiyo kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa na kusema kuwa Kamati hiyo itaendelea kuishauri Serikali kutoa kipaumbele kwa Hospitali ya Kibongóto na kuhakikisha huduma bora zinaendelea kupatikana hapa.
Akijibu hoja ya kwanini Hospitali ya Kibongóto bado haijawa Taasisi kamili, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bw. Tumainieli Macha amesema kuwa Serikali ipo kwenye hatua za mwisho kuifanya Hospitali ya Kibongóto kuwa Taasisi kamili mara baada ya muundo pendekezwa kupitishwa na Mamlaka husika.
“Serikali inashughulikia jambo hili kwa umakini sana na inatambua mchango wa Hospitali ya Kibongóto katika kutoa huduma za tiba pamoja na kufanya tafiti mbalimbali za magonjwa ambukizi na tayari muundo pendekezwa wa Hospitali hii umeshapitishwa na mamlaka husika na tunatarajia kabla ya Bunge la Bajeti miongoni mwa taasisi ambazo zitapitishwa, Hospitali ya Kibongóto itakuwepo”amesema Bw. Macha.
Aidha Bw. Macha ameitaja Hospitali ya Magonjwa ya Akili Milembe pamoja Hospitali ya Rufaa ya Kanda – Mbeya kuwa ni miongoni mwa Hospitali zinazotarajiwa kuwa Taasisi pamoja na Hospitali ya Kibongóto.
Naye Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Dkt. Leonard Subi ameishukuru Kamati hiyo kwa kupokea ombi la Hospitali hiyo kuwa Taasisi na kusema kuwa watumishi katika Hospitali hiyo wanafanya kazi kwa bidii na hivyo kuwaachia watunga Sera hao kuridhia maombi ya Hospitali hiyo kuwa taasisi.
Awali akiwasilisha taarifa ya Hospitali hiyo kwa wajumbe wa Kamati, Dkt. Subi ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha Sekta ya Afya kwa kujenga maabara kubwa ya Afya ya Jamii yenye hadhi ya ‘Bisafety Level 3’ ambayo itagharimu kiasi cha shilingi 11,337,672,870.88 ambapo ujenzi hadi sasa umefikia asilimia 90.
Dkt. Subi amesema Hospitali hiyo kongwe ilianzishwa mwaka 1926 na kwa mwaka huhudumia wastani wa wagonjwa zaidi ya 20,000 ambao kati yao wagonjwa 800 – 1000 huwa ni wagonjwa wa Kifua Kikuu, 150 – 200 huwa ni wagonjwa wa Kifua Kikuu Sugu.
“Huduma za matibabu ya Kifua Kikuu ni bure na wagonjwa huwa wanaletwa hapa na wengine huwa tunawafuata kutoka sehemu mbalimbali kila kona ya nchi hii” Amesema Dkt. Subi.
0 Comments