Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT. GWAJIMA- JITOKEZENI KUPATA HUDUMA ZA KIBINGWA


*************************

Na.WAMJW - Dodoma


Wakazi wa Mji wa Dodoma na vitongoji vyake wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupata huduma za afya kutoka kwa madaktari bingwa waliweka kambi kwenye tamasha la ‘Karibu Dodoma festival ‘ finale endelea kwenye viwanja vya Chinangali jijini hapa.


Wito huo umetolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati akitembelea mabanda ya taasisi mbalimbali yaliyoshiriki tamasha hilo ikiwemo taasisi za afya, Hospitali Maalum, Mkoa na Taifa za wizara hiyo.


Dkt. Gwajima alisema wizara yake imewaletea madaktari bingwa kutoka taasisi na hospitali za Taifa na hivyo huduma zinapatikana ngazi zote kwani matatizo bado yapo kwenye jamii na watu wengi wanatembea na magonjwa bila kufahamu kitu ambacho kinasababisha matatizo Makubwa siku za usoni hivyo akawataka kutumia tamasha hilo kwani huduma imesogezwa.


Akitolea mfano kwenye tamasha hilo amesema kati ya wananchi 67 waliojitokeza kupima maambukizi ya kifua kikuu walipata watu saba wenye kifua kikuu huku mmoja akibainika kuwa na kifua kikuu sugu. Vilevile, baadhi wamebainishwa kuwa na matatizo ya miguu na uti wa mgongo na wamepatiwa vipimo ya X-ray hapohapo kwenye tamasha hilo.


"Hapa kwenye tamasha tunalo gari tembezi la TB ambalo lina Vifaa vyote ikiwemo mashine ya X-ray, wagonjwa wetu wanaofika hapa wanapata huduma za vipimo hapa hapa na hata kama watafika banda la MOI basi vipimo wa kiuchunguzi ya magonjwa ya mifupa na uti wa mgongo watavipata kupitia gari hilo, mie huwa nasema hili gari ni Muhimbili inayotembea” Aliongeza.


Kwa upande wa Ugonjwa wa Saratani Dkt. Gwajima, alisema tamasha hilo limekua na faida kubwa kwani wameweza kuwachunguza akina mama zaidi ya 35 na wanne kati yao wamegundulika na saratani ya shingo ya kizazi na mmoja aligunduliwa kuwa na viashiria vya saratani ya shingo ya kizazi,


”Sasa kama huyu mama asingefika hapa asingejua na baada ya miaka miwili ukute ingekua imeshakomaa na labla asingeweka kufika Ocean road”.


"Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kufikisha huduma karibu na wananchi, tumeona faida kupitia tamasha hili ni wakati sasa wa kupanga kila baada ya miezi mitatu kuwasogezea wananchi huduma hizi huko walipo kwenye mikoa mingine pia watoa huduma wa huko watapata ujuzi zaidi kupitia wataalamu wetu toka hospitali za Taifa kama, Muhimbili,JKCI,MOI na Ocean road”, Alisisitiza.


Aliongeza kwa upande wa maendeleo na ustawi wa jamii Dkt. Gwajima aliwataka wazazi na walezi kuzingatia suala la malezi bora kwa watoto ili kuondokana na watoto wanaoishi mazingira magumu na kufanya kazi mitaani ili Taifa kuwa na vijana wenye msingi na maadili mazuri kwa maendeleo ya nchi.


Hata hivyo aliwaasa wananchi kuacha maamuzi ya kuwapiga watu na kuwanyanyasa wenye matatizo ya afya ya akili kwani kwa sasa wanajipanga kusogeza huduma za hospitali hiyo karibu na wananchi ili kuzuia, kuibua na kupanua huduma za hospitali maalumu ya Mirembe inayoshughulika na afya ya akili.

Post a Comment

0 Comments