******************************
Na WAMJW- MOROGORO.
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima leo amefungua Mkutano wa kujadili taarifa ya tathimini ya utoaji huduma tabibu za kifamasia.
Dkt. Gwajima amefungua Mkutano huo leo Oktoba 27, 2021 Mkoani Morogoro, uliohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa huo na viongozi wengine pamoja na Wataalamu wa afya kutoka Taasisi za Serikali na zisizo za Serikali.
Katika Mkutano huo Dkt. Gwajima amesema kuwa, Wizara kupitia Baraza la Famasi Tanzania imetunga kanuni zinazomwelekeza Mfamasia kutoa huduma za kitabibu za kifamasia kwa wagonjwa hospitalini, huku akiweka wazi kuwa hadi kufikia mwezi Oktoba, 2021 kuna Wafamasia wapatao 2,646 waliosajiliwa.
"Kulingana na rejista ya Baraza la Famasi la Tanzania, hadi kufikia mwezi Oktoba, 2021 kuna Wafamasia wapatao 2,646 waliosajiliwa. Wizara kupitia Baraza la Famasi Tanzania imetunga kanuni zinazomwelekeza Mfamasia kutoa huduma za kitabibu za kifamasia kwa wagonjwa hospitalini."Amesema.
Ameendelea kusema kuwa, Wizara inathamini mchango mkubwa wa huduma tabibu za kifamasia inayotolewa na Wafamasia katika kuboresha tiba ya mgonjwa kwa kushirikiana na jopo la wataalamu wengine wakiwemo Madaktari na Wauguzi.
Aidha, ameweka wazi kuwa, MUHAS imeanzisha utoaji wa mafunzo juu ya huduma tabibu za kifamasia kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili, huku akibainisha kuwa mpaka sasa kuna takribani wafamasia 20 wenye Shahada ya Uzamili ya huduma tabibu za kifamasia hapa Tanzania.
Kwa kutambua umuhimu wa huduma bora ya afya kwa wananchi, Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wote katika Sekta ya Afya wakiwemo Wafamasia kwa kuanza kutambua majukumu yao halisi katika utoaji huduma. Alisisitiza.
Hata hivyo, amesema kuwa, Wizara imepokea mapendekezo ya chama cha kitaaluma cha Famasi kuhusu kuajiri wafamasia wa kutosha katika Hospitali za Rufaa kuanzia ngazi ya Mkoa ili kuboresha huduma hizi.
"Wizara imepokea mapendekezo ya chama cha kitaaluma cha Famasi kuhusu kuajiri wafamasia wa kutosha katika Hospitali za Rufaa kuanzia ngazi ya Mkoa ili kuboresha huduma hizi,"Amesema.
0 Comments