Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Mhe. Tano Mwera (kulia) akiongea na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliofika wilayani kwake kwa ajili ya kufanya kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango 29/10/2021.
Afisa Mkuu Uhusiano kwa Umma wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Mackdonald Mwakasendile (kushoto) akimweleza jambo Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Mhe. Tano Mwera wakati Maafisa wa TRA walipofika wilayani hapo kwa ajili ya kufanya kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango 29/10/2021.
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Mhe. Tano Mwera (aliyevaa kitenge) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliofika wilayani kwake kwa ajili ya kufanya kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango 29/10/2021.
PICHA NA TRA
****************************
MKUU wa Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa, Mhe. Tano Mwera amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya wafanyabiashara Wilayani kwake cha kutotoa risiti za EFD na kuwataka wafanyabiashara hao kujenga utamaduni wa kutoa risiti mara kwa mara pindi wanapouza bidhaa zao.
Kauli hiyo ameitoa leo ofisini kwake wakati alipokutana na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliopo mkoani Rukwa kwa ajili ya kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango.
Mhe. Mwera amesema kwamba, anasikitika kuona kwamba baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wagumu katika kutoa risiti za EFD wakati wanapowauzia bidhaa wateja hali inayopelekea kupoteza makusanyo ya kodi na kuwataka wateja pia wadai risiti wakati wote wanaponunua bidhaa au kupata huduma kutoka kwa wafanyabiashara.
“Kwanini watu hawataki kutoa risiti kabisa, na ukidai risiti ujue unatangaza vita, na kila siku tunasema ukiuza toa risit, ukinunua dai risiti, hii haikubaliki, natoa wito kwa wafayabiashara mutoe risiti na wanunuaji na nyie mdai risiti kila wakati”, alisema Mhe, Mwera.
Ameongeza kuwa, Wilaya ya Kalambo ina fursa nyingi mbalimbali za kiutalii ambazo zinaweza kuinua uchumi na kuongeza mapato ya nchi ikiwemo maporomoko ya Kalambo (Kalambo Falls), bandari ya Kasanga na mpaka wa Kasesya ambao ni kichocheo kizuri cha biashara kati ya Tanzania na Zambia.
Aidha, ameitaka pia TRA kuhakikisha kuwa inaendeleza kampeni ya utoaji elimu kwa wafanyabiashara hao ili waone umuhimu wa kutoa risiti na kutatuliwa kero zao mbalimbali za kibiashara kwa ajili ya kukuza makusanyo ya mapato na kuleta maendeleo nchini kupitia ulipaji wa kodi wa hiari.
Kwa upande wake Afisa msimamizi wa kodi kutoka TRA, Bw. Joel Frael amesema kwamba, agizo la Mkuu wa Wilaya ya Kalambo kwa TRA limechukuliwa na litafanyiwa kazi ambapo naye amehimiza wafanyabiashara kutoa risiti sahihi kulingana na manunuzi ya mteja na kwa wale ambao hawajapata namba za utambulisho wa Mlipakodi (TIN) waende katika ofisi za TRA ili wasajiliwe na kupatiwa TIN.
Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara wametoa maoni yao kuhusiana na kampeni inayofanywa na TRA mkoani Rukwa ambapo wameifurahia na kuiomba TRA kuendelea kuwaelimisha mara kwa mara kwani wengi wao wanaishi pembezoni mwa mji na wana uhitaji mkubwa wa elimu ya kodi.
Kampeni ya elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango kwa sasa iko mkoani Rukwa ambapo kwa siku zijazo itaelekezwa katika Mkoa wa Katavi lengo likiwa ni kutoa elimu ya kodi, kusikiliza kero mbalimbali za wafanyabiashara ili waweze kulipa kodi zao kwa wakati na kwa hiari.
0 Comments