Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI JAFO ASHIRIKI MKUTANO WA KUMI NA NANE WA MAWAZIRI WA MAZINGIRA AFRIKA (AMCEN) KWA NJIA YA MTANDAO



Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo hii leo ameshiriki kwa njia ya mtandao Mkutano wa Kumi na Nane wa Mawaziri wa Mazingira Afrika (Amcen) uliofanyika Jijini Nairobi Nchini Kenya na kuhudhuriwa na Mawaziri wa Mazingira Afrika wapatao 42. Kushoto ni Mhandisi Juma Limbe na Bwana Daniel Sagata kutoka Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais. 

********************** 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo hii leo ameshiriki kwa njia ya mtandao Mkutano wa Kumi na Nane wa Mawaziri wa Mazingira Afrika (AMCEN) uliofanyika Jijini Nairobi Nchini Kenya kwa njia ya mtandao na umehudhuriwa na Mawaziri wa Mazingira Afrika wapatao arobaini na mbili (42) 

Katika mkutano huo mada mbalimbali zimejadiliwa ikiwa ni pamoja na hali ya nchi za Afrika baada ya athari za ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kutekeleza program ya “Africa green stimulus programme” iliyopitishwa na Mkutano Maalumu wa nane wa AMCEN. 

Waziri Jafo amesema Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inatoa msisitizo wa dhati katika agenda ya mazingira kwa maendeleo endelevu. Amesema pia, Ofisi yake inaratibu Kampeni Kabambe ya Kitaifa ya Uhifadhi na Usafi wa Mazingira kwa lengo la kunusuru taifa na majanga yatokanayo na uharibifu wa mazingira. 

Mkutano huu pia umejadili na kuweka mwongozo wa kuimarisha ushiriki wa Afrika katika Mikataba ya Kimataifa inayohusu Hifadhi ya Mazingira hususan Mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi 12 Novemba, 2021, Glasgow, Scotland na Mkutano wa 15 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Hifadhi ya Bioanuai utakaofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 11 - 15 Oktoba 2021, pamoja na Mkutano wa Baraza la Mazingira la Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa utakaofanyika tarehe 28 Februari hadi 2 Machi 2022, Nairobi, Kenya. 

Waziri Jafo amesema Tanzania inapongeza juhudi zinazofanywa na Afrika katika utekelezaji wa African green stimulus programme ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa jukwaa la kimtandao (online platform) kwa ufadhili wa Taasisi ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika. 

Amesema Tanzania inaafiki mapendekezo ya utafutaji fedha ili kusaidia utekelezaji kikamilifu wa African green stimulus programme pamoja na ubadilishanaji wa taarifa na uzoefu kwa maslahi mapana ya Tanzania na Afrika kwa ujumla. Mkutano wa 18 wa AMCEN pia umejadili namna bora ya kuhakikisha sekta ya mazingira inaimarishwa kwa kutoa msukumo zaidi wa kuetelekeza makubaliano yanayofikiwa kwa kuwa yanaweza kuleta athari za kijamii, kiuchumi, kisiasa, kisera, kisheria na kimazingira. 

Aidha, Mkutano huo umepongeza hatua zilizochukuliwa na Kikundi cha Afrika kuhusu Mabadiliko ya tabianchi, kuendelea kusimamia maslahi ya Afrika katika Mkataba wa mabadiliko ya tabianchi na kupitisha ujumbe mahsusi wa Afrika katika Mkutano ujao wa Mabadiliko ya Tabianchi. 

Mkutano huo pia umeunga mkono nia ya nchi ya Misri kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 27 wa Mkutano wa Mabadiliko wa Tabianchi na hivyo nchi wanachama wa AMCEN zinaombwa kushirikiana na Misri katika kufanikisha Mkutano huo. 

Mkutano wa Mawaziri wa Mazingira Afrika (African Ministerial Conference on the Environment (AMCEN) ulianzishwa rasmi mwezi Disemba 1985, ikiwa ni moja ya maazimio ya Mkutano wa Mawaziri wa Mazingira wa Afrika uliofanyika Cairo, Misri kwa lengo la kuhimiza masuala ya hifadhi ya mazingira katika Bara la Afrika; kuhakikisha upatikanaji endelevu wa mahitaji muhimu ya kibinadamu; kuhakikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanapatikana katika ngazi zote; na kuhakikisha kuwa shughuli za kilimo zinakuwa endelevu katika kuleta usalama wa chakula katika jamii.

Post a Comment

0 Comments