******************************
Na Alfred Mgweno (TEMESA)
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) imetenga jumla ya shilingi bilioni 21.4 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vivuko vipya vitano kwa mwaka huu wa fedha 2021/2022 ambavyo vitaenda kutoa huduma katika maeneo mbalimbali ya mito, maziwa na bahari nchini. Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja wa Ujenzi na Matengenezo ya Vivuko kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Lukombe King'ombe wakati akizungumza na waandishi wa Habari kutoka Televisheni ya Taifa (TBC) waliofanya naye mahojiano Mkoani Mwanza katika kipindi maalumu cha Mulika fursa ambacho kinaangazia miradi yote ya Serikali iliyofanyika na ambayo inatarajiwa kufanywa na Serikali kwa mwaka huu wa fedha.
Mhandisi King'ombe amebainisha kuwa miradi hiyo ya ujenzi wa vivuko vipya inatarajiwa kuanza hivi karibuni na itaangazia yale maeneno ambayo yana uhitaji mkubwa zaidi wa huduma za vivuko ambayo ni Nyamisati Mafia Mkoa wa Pwani, Mwanza, Geita pamoja na Kisorya Rugezi Mkoani Mara. Ameongeza kuwa fedha hizo pia zitatumika kwa ajili ya ukarabati wa vivuko ambavyo muda wake wa kufanyiwa ukarabati umefikia, aidha fedha hizo zitatumika kujengea miundombinu ya vivuko ikiwemo majengo ya abiria kupumzika wakati wakisubiri kivuko (Waiting lounge) ambayo yatakuwa na vyoo kwa ajili ya abiria pamoja na kutumika kwa ajili ya ujenzi wa maegesho ya vivuko.
''Kuna maeneo ambayo yana uhitaji wa kuongezewa idadi ya vivuko kama tulivyoona Kigongo Busisi, yale yenye kivuko kimoja kuwa na vivuko viwili ambavyo vinaongeza uwezo zaidi, tutakua na kivuko kipya Kisorya Rugezi, tutakuwa na kivuko kipya cha Nyamisati Mafia, sasa hivi wana kivuko kimoja kwahiyo wanakitegemea hicho na Serikali imeliona hilo, hivyo kupitia ilani ya Uchaguzi tutaongeza kivuko kingine ili kiongeze nguvu kwa wakazi wa Mafia''. Alisema meneja King'ombe.
Mhandisi King'ombe ameongeza kuwa maeneo mengine ambayo Serikali itajenga vivuko vipya kwa mwaka huu wa fedha ni maeneo ya Nyakarilo Kome kwasababu kivuko kinachotoa huduma maeneo hayo cha MV. KOME kwa sasa kina uwezo mdogo na kutokana na kuongezeka kwa watumiaji wa huduma za kivuko, wakazi hao wanahitaji kuongezewa kivuko kingine kipya ili kikidhi mahitaji ya usafiri ya kila siku ya wananchi wa maeneno hayo.
Aidha Mhandisi King'ombe ameongeza kuwa Serikali imepanga kujenga kivuko kipya katika Wilaya ya Magu katika eneo la Ijinga Kahangala, ''ni kivuko ambacho kipo kwenye bajeti ya mwaka huu na tuna kivuko pia kipya kwa ajili ya eneo la Bwira Bukondo, hii ni miradi ambayo itatekelezwa kwa mwaka huu wa fedha''. Amebainisha Mhandisi Kingo'mbe.
Mhandisi King'ombe amewaomba wananchi wanaotumia huduma za vivuko vya TEMESA kuendelea kuuamini Wakala huo kwani una wataalamu wa kutosha ambao wapo kuhakikisha wananchi wanakuwa salama wakati wote wanapotumia huduma za vivuko.
Wakala wa Ufundi na Umeme )TEMESA) unasimamia jumla ya vivuko thelathini na tatu katika vituo ishirini na mbili kote nchini na hivyo ujenzi wa vivuko hivyo ukikamilika itakuwa na idadi ya vivuko thelathini na nane inavyovisimamia.
0 Comments