Na Richard Mrusha
Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeandaa Mpango Mkakati wa Usimamizi wa Masuala ya UKIMWI (VVU) na Kifua Kikuu (TB) katika maeneo ya Migodi.
Mkakati uho uliondaliwa utasaidia upatikanaji wa taarifa sahihi za maambukizi ya magonjwa hayo katika Sekta ya Madini ambapo Utekelezaji wa Mkakati huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2021/2022.
Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Issa Nchasi kwa niaba ya Waziri wa Madini Doto Biteko tarehe 11 Agosti wakati akiwasilisha Taarifa Kuhusu Hali ya Maambukizi ya VVU na Kifua Kikuu katika Maeneo ya Migodi pamoja na Wachimbaji Wadogo wadogo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya VVU na TB Jijini Dodoma.
Nchasi ameieleza Kamati hiyo kuwa Wizara ya Madini kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali imeandaa Mkakati wa kuboresha Mawasiliano na Upatikanaji wa Taarifa juu ya Maambukizi ya VVU na TB kwenye maeneo ya uchimbaji.
"Tume ya Madini kupitia Idara ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kwa kushirikiana na Waganga Wakuu wa Wilaya inaendelea kufanya mafunzo kwa wachimbaji wadogo Mafunzo hayo yanalenga kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali yakiwemo maambukizi ya VVU na TB," amesema Nchasi.
Na Kwa upande wake Waziri Biteko ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kwa ushauri wake makini ambao wamekua wakiutoa katika kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inasimamia afya za wadau wanaojishughulisha na shughuli za uchimbaji madini kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini hususan katika kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kukua kwa kasi na hatimaye kufikia mchango wa asilimia 10 kwenye pato la Taifa ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoelekezwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.
Aidha, Waziri Biteko ameieleza Kamati kuwa mazingira ya uchimbaji mdogo kwenye maeneo yenye leseni na yenye milipuko ya madini (mineral rushes) kwa kiasi kikubwa yanakosa miundombinu wezeshi ya kulinda afya na usalama wa wachimbaji, hivyo Mkakati huu kwa mwaka 2021/2022 utapunguza maambukizi kwa kiasi kikubwa.
Biteko Aliongeza kuwa, wachimbaji kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine kufuatana na uzalishaji wa madini kunachangia ongezeko la maambukizi ya VVU na TB. Biteko amesema Mkakati huu utapunguza maambukizi kwa kiasi kikubwa.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Madawa ya Kulevya na Magonjwa Yasiyo ambukiza (NCD’S) Dkt. Alice Kaijage (Mbunge wa Viti Maalum – Wafanyakazi) ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuandaa Mpango Mkakati kwa ajili ya kupunguza Maambukizi ya VVU na TB katika maeneo ya Migodi pamoja na wachimbaji wadogo.
Dkt. Kaijage ameielekeza Wizara ya Madini kuyatekeleza yote yaliyosemwa kwenye Mkakati huo ili kutoa matokeo kwa wachimbaji. Dkt. Kaijage amesisitiza elimu iendelee kutolewa kwenye maeneo yanayozunguka migodi kuhusu maambukizi ya VVU na TB na kuitaka TACAIDS kuhakikisha inawafikia wachimbaji wadogo kwa uhakika.
Kwa upande wake Nyangusi Laiser kutoka TACAIDS ameieleza Kamati kuwa, wameendelea kutoa elimu kupitia Dawati maalum katika maeneo ya migodi hapa nchini na wachimbaji wadogo ili kujikinga na Maambukizi ya VVU na TB. Amesema wanashirikiana kwa karibu na Wizara ya Madini ili kuhakikisha wanawafikia wachimbaji wengi zaidi wakilenga kutoa mikopo na kondom ili kusaidia.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI imepanga kutembelea migodi mbalimbali hapa nchini ili kujionea shughuli mbalimbali katika maeneo ya migodi pamoja na wachimbaji wadogo ili kutoa elimu na kuhamasisha zaidi kuhusu hali ya Maambukizi ya VVU na Kifua Kikuu.
Waziri wa Madini Dotto Biteko akizungumza kuhusu Hali maambukizi ya vvu na kifua kikuu katika maeneo ya migodi pamoja na wachimbaji wadogo kwa Kamati ya kudumu ya bunge ya maswala ya ukimwi Jijini Dodoma
1 Comments
Mh wazili kazi yako ni nzuri sana mpango huu umelenga magonjwa yanayopunguza nguvu kazi, hivyo nakupongeza sana
ReplyDelete2: swala la ukatili kwa wanawake umelisahau maana hili nalo nisehemu ya mpango kitaifa wanawake wengi hunyimwa haki hunyanuaswa na hawapewi fulsa sawa na wanawake kama kumiliki migodi midogo midogo hasa pale mashaliti yanapokuwa makubwa wanakosa sifa je hili nalo lipo je