Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR MHE.MAZRUI AIPONGEZA BOHARI YA DAWA (MSD)


Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD)’ Meja Jenerali Dkt. Gabriel Saul Mhidze. akiwa ameongozana na Waziri wa Afya wa Zanzibar Mhe. Nassor Ahmend Mazrui wakati akimkaribisha alipotembelea Bohari hiyo jana kujionea shughuli mbalimbali inazozifanya,







Waziri wa Afya wa Zanzibar Mhe. Nassor Ahmend Mazrui akipokea sampuli ya bidhaa za afya zinazo zalishwa na Bohari ya Dawa (MSD) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa MSD’ Meja Jenerali Dkt. Gabriel Saul Mhidze.


Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, akipokea maelezo ya uzalishaji wa dawa kutoka kwa mtaalamu wa Kiwanda cha dawa cha MSD- Keko (Keko Pharmaceutical)


Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui,akiangalia uzalishaji wa Barakoa katika kiwanda hicho.
Msimamizi wa Kiwanda cha Barakoa cha MSD. Bw. Twahil Magooro, akitoa Maelezo ya mchakato wa uzalishaji Barakoa mbele ya Waziri wa Afya Zanzibar.





Na Mwandishi, Wetu


WAZIRI wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mzrui ameipongeza Bohari ya Dawa (MSD) kwa hatua kubwa iliyochukua katika kuanzisha viwanda nchini, kwani itasaidia katika kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini sambamba kuboresha afya za wananchi.


Mhe. Mazrui ametoa pongezi hizo leo tarehe 20/8/2021 baada ya kutembelea Makao Makuu ya Bohari ya Dawa yaliyoko Keko jijini Dar es Salaam, ili kujionea kazi mbalimbali zinazofanywa na Bohari hiyo, mathalani mipango yake ya uzalishaji wa dawa na vifaa tiba.


“Nimevutiwa na hatua za MSD kuamua kuzalisha bidhaa za afya yenyewe, Mkurugenzi Mkuu na Menejimenti ya MSD nawapongeza sana, Sisi kama Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tutaangalia namna tunaweza kushirikiana ili kupanua wigo wa kuboresha huduma za afya. Kiukweli naichukulia MSD kama sehemu ya Wizara ya Afya Zanzibar, “. alisema Mhe. Mazrui.


Katika hatua nyingine Mhe. Mazrui ametembelea viwanda vya MSD ikiwa ni pamoja na Keko Pharmaceuticals na kiwanda cha kuzalisha barakoa na kujionea hatua mbalimbali zilizofikiwa katika uzalishaji, na baadae alitembelea Kanda ya Dar es Salaam huku akipongeza uongozi kwa kazi kubwa zinazofayika na kuwataka kuendelea kujituma ili kuboresha sekta ya afya.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Meja Jenerali Dkt.Gabriel Saul Mhidze ameeleza jitihada mbalimbali alizozifanya toka ateuliwe kushika wadhifa huo, kwani zimesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha huduma za afya nchini.


“Toka nimeteuliwa tumeshirikiana vizuri na Menejimenti yangu kwa pamoja tumejitahidi kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini, ujenzi wa viwanda na mageuzi ya kiutendaji, ninayo Imani kubwa kwamba siku si nyingi, ile adhima ya serikali ya kuboresha afya ya kila mtanzania inaenda kutimizwa kwa kiasi kikubwa kufuatia mageuzi makubwa tunayofanya” alisema Mhidze.


Aidha ameongeza kuwa, ifikapo mwezi wa 10 mwaka huu, Kiwanda cha Mipira ya Mikono, na pamoja na viwanda vingine vya dawa, vinavyojengwa Makambako mkoani Njombe vitaanza kufanya kazi, hivyo kuboresha huduma za upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.


Ameongeza kuwa, kwa dawa na vifaa tiba ambavyo uchakataji wake ni mgumu, tayari MSD imenza kuingia mikataba ya ubia na wazalishaji wa huduma hizo, lengo likiwa ni kupunguza gharama za upatikanaji wa huduma hizo nchini, na kuleta unafuu kwa mwananchi wa kawaida ambalo ndio lengo hasa la serikali.

Post a Comment

0 Comments