Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Balozi wa Oman nchini, Mhe. Ally Abdallah Almahruqi katika hafla ya kumuaga mara baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini. Hafla ya kumuaga imefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amemuaga Balozi wa Oman nchini, Mhe. Ally Abdallah Almahruqi katika ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini.
Balozi Mulamula amempongeza Balozi Almahruqi kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kudumisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Oman na Tanzania wakati wote wa uwakilishi wake hapa nchini.
“Tanzania tunashukuru zaidi kwa ushirikiano uliotuonesha wakati wote ulipokuwa hapa kama Balozi na tunakuahidi kuudumisha na kuuendeleza ushirikiano huo kwa maslahi ya nchi zetu mbili (Tanzania na Oman)," amesema Balozi Mulamula
Kwa upande wake Balozi wa Oman aliyemaliza muda wake wa uwakili hapa Nchini Mhe. Ally Abdallah Almahruqi ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano alioupata wakati wote alipokuwa akitekeleza majukumu yake.
“Nawashukuru sana kwa ushirikiano mlionipatia wakati wote niliokuwa hapa nikitekeleza majukumu yangu kama Balozi, hakika nilifarijika sana……….naahidi kuwa nitakuwa balozi mwema kwa Serikali ya Tanzania,” amesema Balozi Almahruqi
Pia Balozi ameipongeza Tanzania kwa hatua inazochukua za kupambana na virusi vya korona ikiwemo kuungana na mataifa mengine duniani kuchanja chanjo ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.
Tanzania na Oman zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo uwekezaji katika madini, mafuta, gesi, kilimo, usafirishaji, utalii pamoja na biashara.
0 Comments