***********************************
Na. Mwandishi Wetu.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa, amewataka BAKITA kutumia tehama ili kuweza kukuza wigo wa lugha ya Kiswahili katika mataifa mbalimbali duniani ili kuwapa fursa watalaam wa Kiswahili waliopo nchini
“Bakita tumieni njia za kielekroniki sasahivi ulimwengu umehama upo mtandaoni, idara ya Tehama kazeni tumieni mitandao ya kijamii kutangaza fursa za lugha la Kiswahili ili mtu wa nchi za nje akitaka kujifunza kupitia machapisho yenu ajifunze na hii itatoa fursa kwa wataalam wetu kwani kiswahili kwa sasa kina mahitaji makubwa duniani”, Waziri Bashungwa.
Waziri Bashungwa ametoa maagizo hayo leo Agosti 2, 2021 Jijini Dar es Salaam alipofanya ziara katika ofisi za Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na kuwaagiza kuanza kutumia njia mpya yakujitangaza na kutangaza kiswahili nchini na kuachana na mifumo ya kizamani
Pia Waziri Bashungwa aliwataka BAKITA kuangalia fursa za kuanzisha vituo vya mafunzo ya kiswahili katika Balozi mbalimbali Duniani ili Kuunganisha Kiswahili na utalii utakaokuza lugha hiyo ambayo ni ya kumi kati ya lugha zinazozungumzwa sana Duniani pamoja na Utamaduni wa Tanzania.
Katika ziara hii Mhe. Bashungwa alitembelea darasa la kisasa la kufundishia wakalimani lililofungwa vifaa vya kisasa ambalo bado halijafunguliwa rasmi kwa sasa.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa BAKITA, Bi. Consolata Mushi amemueleza Mhe. Waziri kuwa baraza hilo limejipango mwaka wa fedha wa 2021/2022 kuongeza idadi ya wakalimani kufikia 50 nchini ili kukidhi hitaji la ukalimani ili kukidhi tija ya huduma hii nchini.
0 Comments