KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM)Kenani Kihongosi,akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 3,2021 jijini Dodoma kuhusu tamko la BAVICHA la maandamano siku ya tarehe 5 Agosti mwaka huu.
KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM)Kenani Kihongosi,akielezea jambo kwa waandishi wa habari leo Agosti 3,2021 jijini Dodoma kuhusu tamko la BAVICHA la maandamano siku ya tarehe 5 Agosti mwaka huu.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM)Kenani Kihongosi,leo Agosti 3,2021 jijini Dodoma wakati akijibu kuhusu tamko la BAVICHA la maandamano siku ya tarehe 5 Agosti mwaka huu.
...........................................................................
Na.Alex Sonna,Dodoma
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umewataka Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) kuwafunda wanachama wao kwani wamekosa heshima kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 3,2021 jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa UVCCM, Taifa Kenani Kihongosi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tamko la BAVICHA la maandamano siku ya tarehe 5 august mwaka huu.
Kihongosi amesema tamko la Katibu wa BAVICHA John Kambalu la maandamano ya kwenda kudai Mahakama kufuta kesi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe ni kuingilia shughuli za Mahakama kwani Mahakama ni Muhimili unaojitegemea.
"Kwanza Katibu Kambalu tunamtaka aombe radhi kwa vyombo vya ulinzi na usalama na amuombe radhi IGP kipindi mahakama inashughulikia kesi ya Sabaya hao hao Chadema walifurahia na kuipongeza mahakama inapokuja kesi ya Mbowe wanasema anaonewa" amesisitiza Kihongosi
Aidha amewataka wananchi kuacha kutumika kisiasa ifikapo tarehe 5 wakafanye shughuli za kuingiza kipato na kuachana na mandamano ambayo yataliingiza taifa katika machafuko.
"Sisi kama Vijana wa Chama Cha Mapinduzi tuwaambie tu kwamba wananchi kwa sasa wamechoka na siasa zenu za makelele ulafi wa madaraka, siasa za vurugu wananchi wanataka maendeleo kwa sasa"amesema Kihongosi
Kihongosi pia amesema hakuna mtu mwenye mamlaka ya kumtaka Rais atoe tamko kwenye kesi kwani mahakama ni muhimili unaojitegemea na Rais ana miradi mingi ya kushughulikia.
Kadhalika amesema Jeshi limepewa wajibu wa kulinda nchi, na utamaduni wa Tanzania haijawahi kutokea maandamano ya watu kwenda kudai Mahakama kufuta kesi .
Hata hivyo amewataka wananchi kutumia siku hiyo kufanya shughuli zao za kujikwamua kiuchumi na kuachana na wanasiasa wanao washawishi kuandamana.
"Msikubali kutumika kwa wanasiasa walafi na wataka madaraka unaacha shughuli zako za kutafuta ugali wa watoto unaenda kwenye vurugu za maandamano ambazo hazina masilahi kwako ndugu zangu acheni hayo mambo"amesema Kihongosi.
0 Comments