Ticker

6/recent/ticker-posts

UPANUZI WA HOSPITALI TEULE YA MAKIUNGU MKOANI SINGIDA KUGHARIMU SH.10 BILIONI

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge (wa pili kushoto) akipata taarifa wakati wa ziara yake ya kukagua Hospitali Teule ya Makiungu ambayo ipo Wilaya ya Ikungi na Mkoa wa Singida.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge, akizungumza katika ziara hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,Jerry Muro, akizungumza katika ziara hiyo.

Hapa ukaguzi wa Chuo cha Ufundi cha VETA kinachojengwa wilayani Ikungi ukifanyika.

Ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA kinachojengwa wilayani Ikungi ukifanyika.

Ukaguzi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi ukifanyika.

Moja ya jengo la Hospitali ya Wilaya ya Ikungi likiwa katika hatua za kukamilika.







Na Dotto Mwaibale, Singida




UPANUZI wa Miundombinu ya Hospitali Teule ya Makiungu ambayo ni msaada mkubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Ikungi na Mkoa wa Singida kwa ujumla mkoani hapa ambao unaendelea unatarajia kugharimu zaidi ya Sh.10. Bilioni.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Stephen Samanii, wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge wakati wa ziara yake ya kukagua hospitali hiyo iliyoanzishwa Novemba 6,1954, na Askofu Patrick Winters, Mmisionari Mpalotini.

Alitaja baadhi ya majengo yanayotarajiwa kujengwa kuwa ni pamoja na jengo la hudumu za nje (OPD),wodi nane zenye uwezo wa kuwa na vitanda 350, jengo kubwa la upasuaji lenye vyumba sita vya upasuaji kwa wakati mmoja, ukumbi wa mikutano na ofisi za utawala.

Alisema ujenzi huo unatarajiwa kufanyika kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa.

Katika taarifa yake hiyo Dk.Samanii aliiomba Serikali kuisaidia hospitali hiyo msaada wa dharura wa ‘oxygen concentrator’ 10 zisizopungua zenye uwezo wa kuhudumia watu wawili kila moja kwa wakati mmoja.

Pia ameomba msaada wa mitungi ya gesi 20, kwa maelezo kwamba wagonjwa wenye changamoto za kupumua wanaongezeka kila siku hivyo bila ya kupata mitungi hiyo watashindwa kuwahudumia wagonjwa.

“Tunaomba ofisi yako kupitia kwa mganga mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya ya Ikungi, mtusaidie upatikanaji wa vifaa hivyo ambavyo vitasaidia kunusuru maisha ya wananchi”. alisema.

Aidha,ameomba wapatiwe misamaha ya kodi na kuondolewa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), na ushuru wa forodha katika vifaa vya ujenzi, mashine na vifaa tiba.

“Pia vifaa vya usafi (sanitary equipment) vikiwemo vyoo vya kukalia na masinki yake,beseni za pekee,vifaa vya bafuni. na marumaru za square metres 23,000 kwa ajili ya ujenzi unaoendelea. Huo utakuwa mchango mkubwa sana wa serikali yetu katika ujenzi huu wa huduma za afya kwa wananchi wetu”,alisema.

Vile vile Dk.Samanii ameiomba Mamlaka ya Bandari Tanzania (PTA) iruhusu mapema mashine,vifaa tiba na vya ujenzi vilivyokwama bandarini hapo ili kazi hiyo ya ujenzi iweze kuendelea.

“Tunawashukuru kwa namna ya kipekee wafadhili wa nje ya nchi kupitia kwa PD Alessandro Nava na Dk.Manuela Buzzi,.kwa kukubali maombi ya Askofu kufanya kazi hii ya kihistoria,”.alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dk.Binilith Mahenge akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo aliwashukru wafadhili wanaofanya upanuzi wa hospitali hiyo na kuwataka washirikiane na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Ikungi jambo litakalosaidia kupunguza hama kumaliza kero zitakapokuwa zikijitokeza.

“Jambo jingine nawaomba kabla ya kuagiza vifaa au kitu cho chote kutoka nje ya nchi hakikisheni mnaishirikisha ofisi ya mkuu wa wilaya ili waweze kupewa taratibu za kupata msamaha wa kodi au mwingine wowote. Ninawapongeza kwa uamuzi wenu mzuri wa kuiunga mkono serikali katika kuboresha sekta ya afya”,alisema Dk.Mahenge.

Wakati huo huo,Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,Jerry Muro,alisema milango ya ofisi yake itakuwa wazi kwa ajili ya kushirikiana na wafadhili na wadau wa maendeleo ndani ya wilaya hiyo.




Katika ziara hiyo wilayani Ikungi Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge alikagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Hospitali Teule ya Makiungu na Chuo cha Ufundi VETA.

Post a Comment

0 Comments