Na Calvin Gwabara, Mbarali.
SERIKALI Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imeahidi kutoa ushirikiano
ili kufanikisha kupatikana kwa matokeo mazuri ya mradi wa utafiti na kuwezesha
kupatikana kwa suluhisho la changamoto za uharibifu wa mazingira hasa katika
vyanzo vya maji na dakio la mto rufiji na bonde lake lenye mchango
mkubwa katika maisha ya binadamu,mimea na viumbe vingine.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfume
katika warsha ya uzinduzi wa mradi “usimamizi endelevu wa madakio ya maji
kupitia tathmini ya kuimarisha mtiririko wa maji kwa mazingira na utekelezaji
wake katika kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi kutokana na athari
za shughuli za kibinadamu Tanzania” iliyofanyika wilayani humo mkoani Mbeya.
‘’Mimi kama mkuu wa wilaya nina majukumu mengi lakini miongoni mwa
majukumu hayo katika wilaya hii ni kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli za
kiuchumi vizuri na kuboresha maisha yao lakini kuhakikisha nasimamia sheria na
usimaizi wa sheria,kanuni na miongozo mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira jambo
ambalo sio rahisi sana maana wananchi wanahitaji bonde hili kuzalisha mali
lakini pia nisimamie sheria ili kilimo chao kisiathiri mazingira vyanzo vya
maji kwa hiyo ninapambana kuhakikisha nabalansi vitu hivyo viwili kwahiyo ujio
wa mradi huu utanisaidia na kusaidia kusaidia kurahisisha kazi yangu’’
alisema Mfume.
Aidha, nawapongeza watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo SUA na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa
kuanzisha mradi huu wa utafiti na kuona kwamba masuala ya mazingira kama vile
umwagiliaji, kilimo kandokando ya kingo za mito, ufugaji wa mifugo ndani ya
kidakio cha mto Mbarali na Bonde la Rufiji pamoja na ongezeko la watu,
vinasimamiwa kwa uhifadhi kamilifu wa eneo la Magharibi mwa Ukanda wa Bahari ya
Hindi kwamba ni muhimu zaidi kwa ajili ya mtiririko endelevu wa maji
kuelekea Mradi wa Kufua umeme wa Mwalimu Nyerere (Julius Nyerere Hydro Power
Project - JNHPP).’’.
Akizungumzia uharibifu huo Mfume alisema , kuna
masuala mengi ndani ya dakio la Mbarali kama vile ukataji wa miti, kilimo ndani
ya kingo za mto na vyanzo vya maji (Vinyungu), ongezeko kubwa la watu, ufugaji
wa mifugo na skimu za umwagiliaji ambao una matokeo hasi kwenye mtiririko wa
maji, uchafuzi wa mazingira, kupungua kwa ubora wa maji na kuongezeka kwa tope
kunakokwamisha mtiririko endelevu wa maji kwa ajili ya mazingira.
‘’Ni matumaini yangu kwamba mradi huu utakuja na
ufumbuzi wa changamoto zilizobainishwa na kusaidia utekelezaji wa mtiririko
endelevu wa maji kwa mazingira kwenye mto Mbarali kwa mara ya kwanza hapa
Tanzania na Kama Serikali, tunawaahidi kutoa ushirikiano na msaada wowote
unaohitajika katika kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa kikamilifu na kwa
mafanikio makubwa’’ alisema Mfume.
Akitoa neno la
ukaribisho kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa (NEMC) Mhandisi Dkt. Samuel
Mafwenga, Meneja Tafiti za Mazingira kutoka NEMC ambaye pia ni Mtafiti Mkuu
mwenza wa mradi huo Rose Mtui alisema kufuatia majukumu ya utafiti mahususi
ambayo yamefafanuliwa bayana katika Sheria ya Usimamizi wa Mazingira namba 191;
NEMC kwa kushirikiana na taasisi za kitaaluma/utafiti zimekuwa zikitengeneza
miradi/programu na kufanya tafiti na mojawapo ni kama mradi huu
unaozinduliwa leo ili kutatua matatizo mbalimbali ya kimazingira.
‘’Tunajua mazingira na mifumo ikolojia na bioanuai zilizopo (nchi kavu na majini) na huduma zinazopatikana vinaendelea kupata changamoto kutokana na ongezeko la idadi ya watu, matumizi yasiyo endelevu, uchafuzi utokanao na kemikali n.k.. Hii ni muhimu kwa kuwa miradi na program zinalenga katika kuhakikisha rasilimali zote na mifumo ikolijia ambayo watu wanaitegemea kwa maisha inatunzwa’’ alifafanua Mtui.
Akitoa salamu za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Mkurugenzi wa Masomo ya Shahada za juu utafiti uhauwilishaji wa teknolojia na ushauri wa kitaalamu SUA Prof. Esron Karimuribo alisema hivi sasa nchi imeanza kuona matokeo ya uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji kama vile upungufu wa maji yanayotiririka mitoni hasa wakati wa kiangazi,mafuriko wakati wa masika,ubora hafifu wa maji kwaajili ya matumizi ya nyumbani lakini pia matokeo yanayoonekana kwenye ikolojia nyingine za nchi kavu na majini.
‘’Kwa matokeo haya,hatuwezi kuendelea kuyafumbia macho haya yote ambayo yanaleta madhara kwa binadamu,Mifugo,wanyamapori na mazingira hivyo nipende kuwapongeza watafiti kutoka SUA na NEMC kwa kuwa na maono ya kuanzisha mradi huu ambao unakusudia katika utunzaji endelevu wa vyanzo vya maji’’ alisema Prof. Karimuribo.
Prof. Karimuribo aliongeza kuwa SUA inatambua umuhimu wa kusimamia na kuhifadhi vyanzo vya maji na mazingira yake ili yapatikane maji kwa njia endelevu kwa ajili ya kizazi hiki na pia vizavi vijavyo na hivyo akatumia nafasi hiyo kuwakaribisha wale wote wenye sifa na nia ya kujiunga na mwaka huu wa masomo kuomba kusoma SUA na kuwaahidi kuwa hawata jutia hasa ukizingatia ubora wa elimu wanayoitoa Pamoja na umahiri wa watafiti wa chou hicho katika tafiti na kufundisha.
Mtafiti Mkuu wa mradi huo wa utafiti wa EFLOWS Prof. Japhet Kashaigili ambaye pia ni Mratibu wa tafiti na machapisho SUA alisema lengo la warsha hiyo ni kuwafahamisha wadau madhumuni ya mradi huo wa utafiti na matokeo yake,Kujua matarajio ya wadau kutokana na matokeo ya utafiti,Kujua na kuyabainisha majukumu yatakayofanywa na kila mdau katika kuifikia na kuanisha maeneo ya ushirikiano ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa na kuleta matokeo chanya kwa taifa.
‘’Kuna usemi unasema ukitaka kwenda kasi nenda peke yako lakini kama unataka kufika mbali nenda na wenzako usemi huu tunataka kuuzingatia kwa kilahali ili tuweze kupata yote kwa wakati mmoja kwa maana ya kwamba twende kasi ili tufike haraka lakini pia twende Pamoja ili tufike mbali ili utafiti huu uweze kuleta mchango kwa wadau wote kwa manufaa mapana ya taifa, alisisitiza Prof. Kashaigili.
Akitambulisha mradi huo Mratibu wa mradi Dkt. Winfred Mbungu alisema mradi unalenga kufanya utafiti kwenye usimamizi endelevu wa madakio ya maji kupitia tathmini ya kuimarisha mtiririko wa maji kwa mazingira na utekelezaji wake katika kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi kutokana na athari za shughuli za kibinadamu kwenye bonde hilo.
‘’Mradi utajikita
Zaidi kwenye kushirikiana na wadau wote ambao wanahusika kwenye bonde hilo
kwanza kwa kutoa Elimu, kuibua mbinu bora za matumizi na usimamizi salama wa
bonde na kuzipendekeza namna ya kuzitekeleza kwa Pamoja ili mwisho wa siku kila
mmoja ashiriki na kuona thamani ya utunzaji huo wa vyanzo vya maji kwenye bonde
hilo’’ alifafanua Dkt. Mbungu.
Alisema lengo kuu ni kupunguza athari zinazotokana na shughuli za kibinadamu kuongeza uwezo wa kuthamini na kutathimini mtiririko wa mito kwa mazingira kwa kurejesha hali ya mtiririko wa maji ulio endelevu,kufanya tathimini ya mtitirko wa mito kwa mazingira katika Madakio ya mito ili kutoa muongozo wa usimaizi endelevu wa mtiririko wa maji na pia utekelezaji wa mtitiriko uliopendekezwa kwa usimamizi endelevu wa rasilimali za maji.
Dkt. Mbungu alisema mradi huu ni moja ya miradi mitano
inayotekelezwa katika katika nchi tisa kufikia malengo manne ya mradi mama
mkubwa ambao unaitwa WIOSAP ambao malengo yake ni usimamizi wa makazi maalumu
ya viumbe,Kuboresha ubora wa maji ili ifikapo mwaka 2035 maji katika nchi hizo
za mradi yafikie katika viwango vya kimataifa,Usimamizi endelevu wa mtiririko
wa mito na utawala na ushirikiano wa kikanda.
0 Comments