Akizungumza katika hafla hiyo jijini Dar es Salaam leo, Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba, amesema fedha za mkopo huo zitafanikisha utekelezaji wa miradi mitano muhimu kwa huduma za jamii.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa barabara na ujumuishaji wa fursa za uchumi (RISE) wenye thamani ya sh. bilioni 693.2 na mradi wa kuboresha elimu ya juu kwa mabadiliko ya uchumi (HEET) thamani yake ni sh. bilioni 982.1.
Mingine ni mradi wa Tanzania ya kidigitali (DTP), wenye thamani ya sh. bilioni 346.6, mradi wa mabadiliko ya sekta ya nishati Zanzibar (ZESTA) thamani yake ni sh. bilioni 328.1 na mradi wa kukuza ukuaji jumuishi Zanzibar: Maendeleo Jumuishi (BIG-Z) wenye thamani ya sh. bilioni 346.6.
Dk. Nchemba ameeleza kuwa miradi hiyo itawezesha utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa Tanzania ambao unataka kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa malengo ya wananchi.
Amesema utekelezaji huo ni kupitia uboreshaji wa miundombinu, upatikanaji wa nishati wa kuaminika, kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji na kuimarisha mifumo ya elimu za mafunzo.
Amebainisha kuwa mkopo huo ni ishara kwamba serikali ya Tanzania inaaminiwa, hivyo watasimamia fedha hizo kuhakikisha zinatekelezwa katika shughuli lengwa.
Ameeleza kuwa mikataba hiyo iliyosainiwa inaongeza thamani ya miradi iliyofadhiliwa na Benki ya Dunia kufikia Dola za Marekani 5,502.4 na kwamba hivi sasa serikali inakamilisha awamu nyingine ya miradi ya kipaumbele.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho, amesema RISE ni miradi ya barabara jumuishi inayohusisha fursa za huduma za jamii.
“Tunafurahi kuona Benki ya Dunia inatukopesha fedha nyingi kwa mradi huu utakaotekelezwa kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2026,” ameeleza Dk. Chamuriho.
Amefafanua mradi wa RISE utaboresha barabara za vijijini na kutoa fursa za ajira kwa watu katika maeneo yanayopitiwa na miradi yaani Wilaya sita katika Mikoa minne ambayo ni Geita, Tanga, Lindi na Iringa.
“Hii inamaanisha kuwa karibu asilimia 58 ya watu ndani ya kilometa tano katika maeneo ya vijiji vilivyochaguliwa wanaweza kutumia barabara nzuri,” amesema.
Ameongeza mradi huo utajenga uwezo katika usimamizi endelevu wa barabara zinazoboreshwa, ukijumuisha ushirikishwaji wa jamii na utoaji wa fursa za ajira 35,000.
“Tunashukuru mradi huu utashirikisha wananchi wakiwemo wanawake ambapo nilitembelewa na kikundi chao hivi karibuni, sasa hii ni fursa kwao kwakuwa wametengewa asilimia 20 kuonyesha uwezo wao,” amesema.
Amesema kwa upande wa barabara za Mikoa ambazo ndiyo hasa zinahusika na Wizara yake, zitakuwa kilometa 135 na vipaumbele vilivyotumika kuchagua miradi hiyo vimetoka katika Mpango wa Maendeleo ya Kilimo awamu ya pili.
“Tumechagua miradi katika Mikoa inayotoa mazao mengi na Wilaya ambazo zina uzalishaji mkubwa katika shughuli za kilimo, hivyo tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutuletea mradi huu nasi tunamuahidi tutasimamia kwa ukamilifu ili thamani ya fedha ionekane,” amesisitiza.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, amesema mradi huo unalenga kuhakikisha maeneo yote yanafikika na hasa usafirishaji wa mazao vijijini.
“Wizara ya Kilimo walitupa maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa kilimo kwa hiyo mradi huu utatekelezwa katika Mikoa yote 26 ya Tanzania lakini tunaanza na maeneo ya kipaumbele,” amesema.
Ametaja kwa Mkoa wa Iringa watajenga barabara katika halmashauri ya Kilolo, Mufindi na Iringa Vijijini na Mkoa wa Lindi ni katika Halmashauri ya Ruangwa na Mkoa wa Tanga ni Halmashauri ya Handeni Vijijini.
Amesema katika kuchagua maeneo ya vipaumbele waliangalia idadi ya watu, idadi ya magari, usafirishaji wa mazao, muunganiko na ukuaji wa huduma za jamii na kwamba mradi huo unaanza kutekelezwa mwaka huu.
Ameongeza kuwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), watajenga barabara zenye urefu wa kilometa 400, pia kutakuwepo na matengenezo ya barabara kilometa tano vijijini ambapo vikundi vya watu wanaoishi katika maeneo husika ndivyo vitakavyotumika.
“Tunataka kuona ushiriki wa wanawake katika utekelezaji wa mradi huo na tumesema angalau asilimia 20 ya vikundi viwe wanawake na nawataka Wakurugenzi wa Halmashauri husika kuwapa mikopo wanawake ili wanunue zana za utekelezaji wa kazio hizi pasiwe na kisingizio,” amesema.
Profesa Joyce Ndalichako ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, amesema mradi wa HEET unalenga kuendeleza elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi.
Ameeleza katika mradi huo wataboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika taasisi za elimu ya juu na kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na soko la ajira.
Kwa upande wake Jamal Kassim Ally ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, amesema miradi hiyo itakayoigusa Zanzibar itakuwa kichocheo kikubwa cha maendeo ya visiwa hivyo.
Amesema kupitia mradi wa umeme utawezesha kujenga mitambo ya umeme wa upepo utakaozalisha Kilovoti 18 na hivyo kupunguza adha ya kukatika kwa umeme hasa katika maeneo ya utalii.
Kuhusu ujenzi wa miundombinu, amesema mradi huo utajenga barabara katika Mji Mkongwe na maeneo ya pembezoni hivyo kurahisisha usafiri kwa wakazi na watalii.
Naye Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia Dk. Faustine Ndugulile, ametaja mradi wa Tanzania ya kidigitali utasaidia kuboresha mazingira ya mtandao kwa watanzania na uwezo wa serikali kutoa huduma za kidigitali kwa umma.
0 Comments