Na Dotto Mwaibale, Singida
SERIKALI imekamilisha ujenzi wa mradi wa maji wenye gharama ya zaidi ya Sh.192.7 Milioni uliotekelezwa katika Vijiji vya Dung'unyi na Munkinya wilayani Ikungi mkoani Singida.
Akizungumza na waandishi wa Hmhabari jana Afisa Mtendaji Kata ya Dung'unyi, Yahaya Njiku alisema kukamilika kwa mradi huo kutawaongezea kasi ya maendeleo wananchi wa vijiji hivyo ambao walikuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya kazi za uzalishaji.
Alisema mradi huo utawanufaisha wananchi zaidi 4946 wa vijiji hivyo ambao sasa wameondokana na adha waliyokuwa wakiipata ya kukosa maji.
Akizungumzia ujenzi wa mradi huo Njiku alisema unahusisha tenki la maji lenye ujazo wa lita 50,000 ambalo limejengwa kwenye mnara wa mita 12.
Alisema chanzo cha maji cha mradi huo ni kisima chenye uwezo wa kutoa 4,800 lita kwa saa, mtandao wa mabomba unaofikia kilomita 5.6 huku kukiwa na jumla ya vituo saba vya kutolea maji.
"Mradi huu umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi hivi sasa wameanza kupata huduma ya maji wakati tukisubiria uzinduzi wake rasmi,". alisema Njiku.
Njiku ameipongeza Serikali kwa kumaliza mradi huo kwa wakati na akatumia nafasi hiyo kumshukuru Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Ikungi Mhandisi Hoppeness Liundi kwa kuwashirikisha viongozi wa Serikali na wananchi katika kutekeleza mradi huo ambao ni mmoja kati ya miradi mikubwa wilayani humo.
Njiku amewataka wananchi wa vijiji hivyo kulinda na kutunza miundombinu ya mradi huo na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka fedha za miradi katika wilaya hiyo.
Njiku ametoa onyo kwa mtu yeyote atakaebainika anahujumu miundombinu ya mradi huo na kuwa Serikali haitasita kumchukulia hatua kali za kisheria.
Aidha Njiku amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu kwa kuwasemea bungeni wananchi wa Kata ya Dung'unyi jambo lililosaidia kupatikana kwa mradi huo katika vijiji hivyo na Kijiji cha Kipumbuiko.
Wakazi wa vijiji hivyo wakiongea kwa nyakati tofauti wameishukuru Serikali kwa kuwakamilishia mradi huo na kueleza kuwa walikuwa na changamoto kubwa ya maji kwani walilazimika kwenda kuchota kwenye visima vya kienyeji na madimbwi ya maji ya mvua.
Theresia Mghesi Mkazi wa Kijiji cha Dung'unyi alisema wanawake ndio waliokuwa wakihangaika usiku na mchana kufuata maji umbali mrefu wa zaidi ya kilometa saba hali iliyosababisha wakati mwingine ndoa zao kutetereka.
0 Comments