Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Iringa
Serikali imekamilisha mazungumzo na kampuni ya ubia ya Saudi Sudani kwa ajili ya kuuza unga pamoja na mtama mweupe.
Hiyo ni fursa kubwa kwa wafanyabiashara nchini kwani wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo ambayo itakuwa sehemu ya muarobaini wa soko la nafaka kwa wakulima nchini.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 2 Agosti 2021 mjini Iringa mara baada ya kutembelea na kukagua kinu cha usagaji nafaka cha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB).
Kuhusu kadhia ya uzalishaji duni wa mazao mbalimbali hususani nafaka Waziri Mkenda amesema kuwa serikali inaendela kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kuongeza tija kwenye mazao kadhalika kuongeza uzalishaji.
“Kuna uwezekano wa kuzalisha gunia 40 katika hekari moja hivyo ni lazima tuweke msisitizo kwenye kuongeza uzalishaji na tija” Amekaririwa Waziri Mkenda
Amesema kuwa pamoja na kuongeza tija na uzalishaji lakini ili kufikia hatua kubwa katika uzalishaji na tija hivyo ni lazima kuimarisha sekta ya mbegu na kuwa na upatikanaji wa mbegu bora nchini.
Kuhusu bei ya mahindi, Prof Mkenda amesema kuwa bei ya mahindi iliporomoka hivi karibuni ambapo aliagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) pamoja na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) kuingia sokoni ili kununua nafaka hususani mahindi jambo ambalo limeanza kuimarisha bei ya mahindi.
Katika ziara hiyo ya Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda kwenye mikoa ya Nyanda za juu kusini imejikita katika kugagua hali ya upatikanaji wa mbolea, ununuzi wa mahindi pamoja na kukagua skimu za umwagiliaji.
0 Comments