Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Iringa
Serikali imebainisha kuwa suluhisho
pekee la sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji ni kuongeza uwezo wa kiuhandisi katika
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof
Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 2 Agosti 2021 mara baada ya kutembelea
na kukagua Skimu za Umwagiliaji za Magozi na Mkombozi zilizopo katika Tarafa ya
Pawaga katika Wilaya ya Iringa Mkoani Iringa.
Amesema kuwa Serikali
imekusudia kufanya hivyo ili kuongeza ufanisi wa kazi katika Tume hiyo ya Taifa
ya Umwagiliaji jambo litakaloimarisha kilimo cha Umwagiliaji ili wakulima
waachane na Kilimo cha kutegemea mvua za msimu.
Kadhalika ili kutatua
changamoto mbalimbali kwenye Skimu za Umwagiliji, Waziri Mkenda amesema kuwa serikali
imekuja na suluhisho ambalo ni mpango
shirikishi kwa watumia maji.
Amebainisha kuwa mpango huo
itakuwa ni kutoza tozo kwa watumia maji ili kukiwa na matatizo ya uharibifu wa
miundombinu Mfuko huo maalumu uweze kutumika kwa ajili ya marekebisho hayo.
Pamoja na mambo mengine Waziri
Mkenda ametoa rai kwa wakulima kote nchini kuhakikisha kuwa wanaendelea na
shughuli za uzalishaji mali ikiwemo Kilimo lakini wanapaswa kuchukua tahadhali
zote zinazoelekezwa na serikali ili kujiepusha na maambukizi ya UVIKO 19.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof
Adolf Mkenda ameanza zira ya kikazi katika mikoa ya Nyanda za juu kusini Iringa,
Njombe, Songwe na Rukwa ambapo atakagua hali ya upatikanaji wa mbolea, ununuzi
wa mahindi pamoja na kukagua skimu za umwagiliaji.
MWISHO
0 Comments