Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kumsimamia mkandarasi Proactive Independent Group anayejenga Daraja la Mbaka lenye urefu wa mita 40 kukamilisha ujenzi wa daraja hilo ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Ameongeza kuwa Serikali haitamuongezea muda mwingine mkandarasi kukamilisha kazi za daraja hilo kwa mwaka ujao kwani daraja lililopo hivi sasa halina uwezo wa kubeba magari makubwa yenye uzito mkubwa na hivyo wananchi wanauhitaji mkubwa wa daraja hilo.
Aidha, Mhandisi Kasekenya ameongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu hiyo kutaharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika wilaya ya Rungwe na Busokelo kwani kutaboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji wa abiria pamoja na mazao yanayopatikana kama vile Kokoa, Parachichi, Tangawizi, Ndizi, Maweze, n.k
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya amekagua matengenezo ya barabara kuu inayoanzia Uyole hadi Kasumulu yenye urefu wa kilometa 102.5; sehemu ya Ilima (km 3) ambapo imekuwa ikifanyiwa matengenezo ya mara kwa mara kutokana na uwepo wa maji mengi ya mvua kutoka milimani na kuridhishwa na maendeleo yake.
“Nimeridhishwa na ujenzi wa kipande hiki cha kilometa tatu ambao umeanza mapema kabla ya msimu wa mvua kuanza kwani mmeamua kukijenga upya kipande hiki kwa kuweka mifumo itakayoweza kupitisha maji kwa chini bila kuathiri tuta la barabara lakini pia kujenga mitaro mikubwa na kutatua tatizo la eneo hilo”, amefafanua Naibu Waziri Kasekenya.
Naye, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Mbeya, Mhandisi Given Njiro, amemuahidi Naibu Waziri Kasekenya kuwasimamia wakandarasi hao wanaoendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja katika mkoa wake kikamilifu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Dkt. Vincent Anney, amemshukuru Naibu Waziri Kasekenya kufika mpaka wilayani kwake na kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja pamoja na barabara na kumuahidi kuendelea kusimamia kwa karibu miradi hiyo.
Mkuu wa Wilaya huyo ametoa wito kwa TANROADS kumsimamia mkandarasi huyo katika kuhakikisha ajira zinatolewa kwa wazawa wa maeneo ya mradi kwanza ili kuongeza pato la wananchi na kuilinda miundombinu hiyo.
Mbunge wa jimbo la Kyela, Mheshimiwa Ally Jumbe, ameishukuru Serikali Awamu ya Sita kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara, madaraja na bandari, kwani itainua shughuli za kiuchumi katika jimbo lake na Mkoa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mbeya, Mhandisi Given Njiro, wakati akikagua ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Bujesi - Mbambo (km 11.7) na Kibanja – Tukuyu (km 7), mkoani humo .
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Dkt. Vincent Anney (kulia), akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa Daraja la Mbaka (m 40) linalohudumia wananchi wa Kyela, Tukuyu na Rungwe, mkoani Mbeya.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Mbeya, Mhandisi Given Njiro (kushoto), akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Bujesi - Mbambo (km 10) kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati alipokagua kazi za ujenzi zinazoendelea katika mradi huo.
Muonekano wa hatua za ujenzi wa Daraja la Mbaka lenye urefu wa mita 40, ulipofikia ambapo mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 69.6 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (mwenye shati jeupe) akipita juu la Daraja la zamani wakati akikagua ujenzi wa Daraja la Mbaka (m 40), ambao ujenzi wake umefikia asilimia 69.6. Daraja hilo litakapokamilika litachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Kyela, Tukuyu na Rungwe, mkoani Mbeya.
0 Comments