Na. Veronica E. Mwafisi-Dodoma
Tarehe 20 Agosti, 2021
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael amesema, Mwongozo wa Tathmini ya Mahitaji ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma unaoandaliwa na Serikali utaziwezesha Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Mamlaka za Serikali kuandaa mpango wa mafunzo utakayozingatia mahitaji halisi ya Watumishi wa Umma kujengewa uwezo kwa lengo la kuwaongeza ufanisi kiutendaji.
Dkt. Michael amesema hayo, wakati akifungua kikao kazi cha wadau kujadili Rasimu ya Mwongozo wa Tathmini ya Mahitaji ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa, Ofisi ya Rais – UTUMISHI kupitia Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu imeandaa rasimu ya Mwongozo wa Tathmini ya Mahitaji ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma ambao uboreshaji wake unategemea maoni ya wadau walioshiriki kikao kazi hicho cha kuijadili rasimu hiyo ili iendane na mahitaji ya Watumishi wa Umma na Serikali kwa ujumla.
Dkt. Michael ameongeza kuwa, pindi mwongozo huo utakapokamilika utaziwezesha Taasisi zote za Umma nchini kuandaa mpango wa mafunzo utakaozingatia mahitaji ya Watumishi na hatimaye kuwa na manufaa katika maboresho ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Mwongozo utawasaidia waajiri kuwapatia watumishi mafunzo stahiki ikiwa ni pamoja na kuiwezesha Serikali kufanya matumizi sahihi ya fedha za umma katika eneo la mafunzo,” Dkt. Michael amefafanua.
Akitoa maelezo ya awali kuhusu kikao kazi hicho, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Balozi Msafiri Marwa amesema, lengo la kikao kazi hicho ni kujadili na kupokea maoni kwa ajili ya kuboresha Rasimu ya Mwongozo wa Kufanya Tathmini ya Mahitaji ya Mafunzo katika Utumishi wa umma.
Balozi Marwa amesisitiza kuwa, mwongozo huo utarahisisha namna ya kufanya tathmini na kufahamu mahitaji halisi ya mafunzo katika Taasisi za Umma kwani mafunzo ni muhimu katika kuendeleza rasilimaliwatu itakayoziwezesha Taasisi za Serikali kufikia malengo.
“Mwajiri akitoa mafunzo kwa watumishi wake bila kujua na kuzingatia mahitaji halisi anaweza asipate matokeo anayoyatarajia, ikiwa ni pamoja na kupoteza muda na fedha za umma, hivyo mwongozo ukikamilika utakuwa nguzo muhimu sana kwa taasisi za umma katika utoaji wa mafunzo,’’ Balozi Marwa amesisitiza.
Kwa upande wake Afisa Mahusiano Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Irene Cidosa, ambaye ni mshiriki wa kikao kazi hicho, amesema Mwongozo wa Tathmini ya Mahitaji ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma ni muhimu kwa sababu itaondoa changamoto ya kila taasisi kutekeleza majukumu tofauti na nyingine.
“Kwa kuwa dunia inabadilika ni lazima watumishi kila wakati wawe na ujuzi unaoendana na wakati uliopo ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu,” Bi. Cidosa amehimiza.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kutambua mchango wa rasilimaliwatu katika maendeleo ya taifa, imeandaa kikao kazi cha wadau kujadili Rasimu ya Mwongozo wa Tathmini ya Mahitaji ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma ili kupokea maoni yatakayoboresha mwongozo huo ambao waajiri watautumia kutoa mafunzo yenye tija kwa taifa.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akizungumza na wadau wa Wizara, Taasisi za Umma na Idara zinazojitegemea wakati akifungua kikao kazi cha kujadili Rasimu ya Mwongozo wa Tathmini ya Mahitaji ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.
Baadhi ya wadau wa Wizara, Taasisi za Umma na Idara zinazojitegemea wakiwa katika kikao kazi cha kujadili Rasimu ya Mwongozo wa Tathmini ya Mahitaji ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.
Baadhi ya wadau wa Wizara, Taasisi za Umma na Idara zinazojitegemea wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael (hayupo pichani) alipokuwa akifungua kikao kazi cha kujadili Rasimu ya Mwongozo wa Tathmini ya Mahitaji ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa Wizara, Taasisi za Umma na Idara zinazojitegemea baada ya kufungua kikao kazi cha kujadili Rasimu ya Mwongozo wa Tathmini ya Mahitaji ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.
0 Comments