Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imepongeza uwekezaji mkubwa katika elimu uliofanywa na Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM) Dk. Jasson Rweikiza hali ambayo imesaidia watanzania wengi kupata elimu na ajira.
Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, Kheri James kwenye mahafali ya 18 ya shule ya St Anne Marie Academy ya Mbezi Kimara kwa Msuguri, shule ambayo inamilikiwa na mbunge huyo.
Alisema uwekezaji huo mbali na kusaidia katika elimu umetoa ajira nyingi kwa watanzania hivyo kupungzua tatizo la ajira nchini kwa kuajiri walimu wengi, madereva, walinzi, watendaji wa mazingira ambao jumla wanafikia 200.
“Hili ni jambo kubwa sana kwetu serikali lazima tumtie moyo ili aendelee na jitihada zake za kuwekeza kwenye sekta ya elimu na tunaomba watanzania wengi waige mfano huu ili watanzania wengi waweze kupata elimu,” alisema Kheri
Mkuu wa Wilaya aliwapongeza wanafunzi hao wa darasa la saba ambao alisema matokeo yanaonyesha kuwa wamefanya vizuri sana kwenye matokeo yao ya mtihani wa utimilifu Mkoa wa Dar es Salaam na mitihani ya majaribio ya darasani yaliyokuwa yakifanyika kwenye shule hiyo.
“Nimesikia kwenye taarifa mbalimbali kwamba mlikuwa na nidhamu sana darasani na mlisoma kwa bidii sana sasa kwa mwenendo huo ni matumaini yangu kwamba mtafanya vizuri sana kwenye mitihani yenu ya kitaifa mnayotarajia kuifanya mapema mwezi Septemba,” alisema
Alisema shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma kwa kuongoza kwenye Wilaya ya Ubungo na Mkoa wa Dar es Salaam kwa miaka minne mfululizo matokeo ya darasa la saba yamekuwa mazuri.
Mkuu wa shule hiyo, Gladius Ndyetabura alisema kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka 2017, shule hiyo ilikuwa ya kwaza Wilaya ya Ubungo, ya kwanza Mkoa wa Dar es Salaam nay a nane kitaifa na mwaka 2018 ilikuwa ya kwanza Wilaya ya Ubungo, ya kwanza Mkoa wa Dar es Salaam na ya sita kitaifa.
Alisema mwaka 2019 shule hiyo ilikuwa ya kwanza tena Wilaya ya Ubungo na ya kwanza Mkoa wa Dar es Salaam huku ikishika nafasi ya 13 kitaifa na kwa mwaka 2020 ilikuwa ya kwanza Ubungo, ya kwanza Mkoa wa Dar es Salaam na ya nane kitaifa.
Alisema kwenye matokeo ya mtihani wa moko darasa la saba mwaka huu wanafunzi wote walipata alama A kwenye masomo yote hivyo kuwa ya kwanza kwa Mkoa wa Dar es salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kheri James (wa pili kulia) akikabidhi cheti kwa mwanafunzi wa darasa la saba shule ya St Anne Marie Aacademy ya Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam, Shigongo Ndaki, aliyefanya vizuri somo la stadi za kazi kwenye mahafali ya 18 yaliyofanyika mwisho mwa wiki shuleni hapo. Kulia ni Mkurugenzi wa shule hiyo, Dk. Jasson Rweikiza na kushoto ni Mkuu wa shule Gladius Ndyetabura
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kheri James (wa pili kulia) akikabidhi cheti kwa mwanafunzi wa darasa la saba shule ya St Anne Marie Asimwe Mwemezi, aliyefanya vizuri somo la stadi za kazi kwenye mahafali ya 18 yaliyofanyika mwisho mwa wiki, mkoani Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa shule hiyo. Galdius Ndyetabura na kulia ni Mkurugenzi wa shule hiyo, Dk. Jasson Rweikiza
Wanafunzi wa shule ya St Anne Marie wakionyesha mfumo wa antena inavyofanya kazi ya kupeleka mawasiliano kwenye TV kwenye mahafali ya 18 yaliyofanyika mwisho mwa wiki mkoani Dar es Salaam
Wanafunzi wa shule ya St Anne Marie aavcademy ya Mbezi Kimara wakifurahi baada ya mahafali ya 18 kumalizika yaliyofanyika shule hapo mwisho mwa wiki mkoani Dar es Salaam
0 Comments